Na Ali Abass
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, kipo mbioni kuanzisha Shahada ya Elimu kwa Michezo na Sayansi ya Michezo (Bachelor of Education in Physical Education and Sports Science ) itakayo saidia kuimarisha nafasi ya ushirikishwaji wa michezo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, msingi na sekondari
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Skuli ya Elimu SUZA, Dkt, Said Khamis Juma, huko ofisi kuu za SUZA Tunguu, wakati alipokutana na ujumbe wa vyuo vikuu vya, OULU na UEF ,kutoka nchini finland pamoja na wajumbe wa mashirika ya Sport and Development Aid (SDA ) na LIIKE Sport and Development, ulioongozwa na Bi. Niina Loukkola.
Akizungumza na ujumbe huo Dkt. Said, alisema program hiyo inalenga kuinua vipaji vya wanafunzi, kuimarisha afya ya mwili na akili na kuongeza mashirikiano baina ya wanafunzi wa SUZA na wanafunzi wa vyuo vyengine vya ndani na nje ya nchi.
Dkt. Said aliuweleza ujumbe huo kuwa SUZA tayari imeshaanda mazingira ya kufundishwa Kozi hiyo amabayo mwaka wa Masomo wa 2026/2027, itaanza kusomeshwa rasmin chuoni hapo
Aidha aliwataka wanafunzi watakao shiriki mafunzo yatakayotolewa na wataalamu hao kusikiliza kwa makini na kuyafanyia kazi kwa vitendo ili yaweze kuleta athari chanya kwao na jamii kiujumla.
Kwa upande wake Bi. Niina Loukkola Kutoka Chuo Kikuu cha OULU , alisema ziara hiyo inalenga kuimarisha michezo kwa wanafiunzi wa vyuo vikuu, kuongeza uelewa na kuonesha fursa zinazopatikana kutokana na ushiriki wa michezo kwa wanafunzi
Nae Mjumbe kutoka Taasisi ya SDA, Bi Miia Hautakangas alisema michezo inahamisisha shuhuli mbali mbali za kijamii ikiwemo, usafi wa mazingira, kuondosha umasikini, kuweka haki sawa, kuwa rafiki na mabadiliko ya tabianchi na usawa wa kijinsia ,ambapo wanamichezo hutumia fursa hiyo kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na njia za kujitengezea kipato.
Akizungumizia kuhusiana na ushirikishwaji sawa wa kijinsia (Gender Equality) Bi.Lumi Twinnine kutoka Chuo Kikuu Cha Eastern Finland, alisema wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo rasilimali,vifaa vya michezo, uwezo wa kujiendesha, nafasi ya uongozi na ukosefu wa kuto kutangazwa na vyombo vya habari suala linalo warejesha nyuma katika ushiriki wa michezo.
Ujumbe huo utatoa mafunzo ya michezo mbali mbali ya nadharia na vitendo kwa wanafunzi kuanzia leo tarehe 20/01/2026 hadi 23/01/2024.


0 Comments