6/recent/ticker-posts

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo akagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Zanzibar Sports City



 Wilaya ya Magharibi 'B' 21/01/2026


Waziri  wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Zanzibar, Mhe. Dk. Riziki Pembe Juma, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Zanzibar Sports City unaoendelea katika eneo la Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi,

 Amesema Ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya maandalizi ya Michezo ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na Mikakati ya kuimarisha miundombinu ya michezo na kuongeza uwezo wa Zanzibar kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa. 

Alieleza kuwa ujenzi huo unalenga kuiweka Zanzibar katika ramani ya michezo barani Afrika na duniani kwa kuwa na viwanja vinavyokidhi viwango vya kimataifa.vinavyozingatia Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Waziri huyo alisema utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya jitihada za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika kuhakikisha sekta ya michezo inapewa kipaumbele, hususan kwa lengo la kuinua pato la vijana wanamichezo na kukuza utalii wa ndani na wa kimataifa kupitia michezo.

Akizungumza kwa niaba ya msimamizi wa mradi kutoka Kampuni ya Orkun Group, Mhandisi Abdulhamid Mhoma alisema uwanja huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 36,500. 

Alisema hadi sasa ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 30, huku pia kukiwa na viwanja viwili vya ziada vya mazoezi vitakavyojengwa pembeni ya uwanja mkuu pamoja na eneo maalumu la gwaride.

Alifafanua kuwa ndani ya miezi mitatu ijayo, kazi za utengenezaji wa sehemu kubwa ya viti vya watazamaji zinatarajiwa kufikia hatua ya juu, hali itakayotoa taswira ya jumla ya uwanja huo.


Imetolewa na Kitengo cha Habari .
WHSUM.

Post a Comment

0 Comments