ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuwa jukwaa muhimu linalolenga kuimarisha juhudu za pamoja za kuimarisha afya za wanawake barani Afrika.
Akifungua Kongamano la tano wa Afya ya wanawake Afrika, uliofanyika katika ukumbi wa Madinatul Bahar Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema kuwa afya ya wanawake ni muhimili wa maendeleo ya familia, Uchumi,ustawi wa jamii na kusisitiza kuekeza zaidi katika kinga, uchunguzi wa mapema ili kuondokana na maradhi mbali mbali yanayoweza kutibika.
Amefahamisha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana barani Afrika ikiwemo Zanzibar, bado kunakabiliwa na changamoto za maradhi mbali mbali yakiwemo saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti na vifo vitokanavyo na uzazi na upatikanaji mdogo wa huduma za afya kwa wanawake.
Amesema kwa Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, imefanya uwekezaji mkubwa ikiwemo Taasisi ya Saratani Zanzibar, itakayotoa huduma za kisasa za uchunguzi, matibabu, mafunzo na utafiti wa maradhi hayo sambamba na kujenga Hospitali 10 za Wilaya na Mkoa na kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi.
Dkt Mngereza ametoa wito kwa nchi za Afrika kuendelea kuimarisha ushirikiano katika suala zima la huduma za Afya kwakufanya tafiti mbali mbali za Afya ili kuweza kufikia lengo la huduma za Afya kwa wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt Salim Slim amesema kuwa katika kuimarisha huduma za Afya wanaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali kwa hatua za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kuweka miindombinu iliyobora kuanzia vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya na Mkoa sambamba na kuwapatia mafunzo wataalamu wa sekta ya Afya.
Amesema mkutano huo uliwakutanisha wataalamu mbali mbali katika nchi za Afrika ni muhimu na utasaidia kuimarisha Afya za wazanzibari katika nyanja tofauti na wataalamu wa Zanzibar n awa nchi nyengine watapata kubadilishana uzoefu walionao.
Kwa upande wake Mkurugenzi mradi wa saratani ya matiti katika Taasisi ya Jhpiego na Msaidizi Mwenyekiti katika kongamano la tano la wanawake Afrika Dkt Mary Rose Giattas amesema mkutano huo malengo yake makubwa ni kutoa nafasi kwa wahudumu wa Afya na wataalamu wa Afya wa Zanzibar na wataalamu wengine kutoka nchi za Afrika kujifunza katika maeneo ya mbali mbali yakiwemo maradhi ya kuambukiza na yasioyakuambukiza.
Amefahamisha kuwa maeneo mengine wanayojadiliana ni kuhusiana na afya mama na mtoto, huduma za chanjo hasa kwa wasichana pamoja na huduma za dharura ambapo kwa nchi nyingi za Afrika zinafanya vizuri katika huduma hiyo na kuendelea kutengeza uhusiano mzuri baina ya Zanzibar nan chi hizo.
Nae Mkuu wa Skuli za Afya na Sayansi za Tiba wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake na kizazi Dkt Salma Abdi Mahmoud amesema kuwa wamefarajika kupata ugeni wa madaktari bingwa wa fani tofauti kutoka nchi za Afrika ambapo watapa kujifunza na kutoa changamoto zinazowakabili nchi husika na kuwapa mbinu za kuzitatua.




0 Comments