Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar, Daktar Ulfat A. Ibrahim, pamoja na watendaji wake, wamefanya ziara ya kukagua maktaba katika skuli mpya zilizofunguliwa hivi karibuni na zilizotangulia hapo nyuma. Ziara hiyo imeanza na skuli za Mjini Magharib, zikiwemo Skuli ya Wasichana Benbella, Tumekuja na Skuli ya Muungano.
Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha huduma za maktaba katika skuli hizo na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata fursa ya kusoma na kujifunza kwa urahisi. Daktar Ulfat amesema kuwa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar imejipanga kufanya mapinduzi ya kifikra juu ya maana, matumizi, na umuhimu wa maktaba na wakutubi katika kufikia malengo ya elimu Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Bodi Ya Huduma Za Maktaba Zanzibar, amepokea maelezo kutoka kwa watendaji wa skuli hizo wakiwemo wakutubi kuhusu changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma za maktaba. Amesema kuwa Bodi ya Huduma za Maktaba Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa skuli zote ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata huduma bora za maktaba.
Imetolewa Katika Kitengo Cha Uhusiano - Bodi Ya Huduma Za Maktaba Zanzibar
BOHUMAZA



0 Comments