6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR- KUFTARI NA WANANCHI WA JIMBONI KWAKE --- KIWANI

Mwakilishi wa jimbo la Kiwani ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi, watoto yatima pamoja na Wananchi wa Jimbo la Kiwani mara baada ya  Iftari aliyowaandalia iliyofanyika Nyumbani kwake Kiwani Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Mwakilishi wa jimbo la kiwani Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka wananchi wa jimbo la kiwani kudumisha umoja, upendo na  mshikamano baina yao ili kuwawezesha viongozi kutimiza malengo yao.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na Viongozi, watoto yatima pamoja na Wananchi wa Jimbo la Kiwani mara baada ya  Iftari aliyowaandalia iliyofanyika Nyumbani kwake Kiwani Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba. 

Amesema suala la umoja na mshikamano ndio nyenzo pekee ambayo itapelekea kutimiza malengo waliojiwekea ikiwemo kuwasaidia watu wasiojiweza na wenye mahitaji maalumu waliomo jimboni humo.

Alhajj Hemed amesema ameamua kuftari na watoto yatima zaidi 100 waliomo jimboni humo kwa lengo la kuwaweka karibu na kudumisha upendo ili nao wajione sawa na watu wengine.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka Wananchi wa kiwani na watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo   jimbo la kiwani ni miongoni mwa wanufaika wa miradi hio.

Amesema Amani na mshikamano ndio chachu ya maendeleo nchini, hivyo kila mtu kwa nafasi yake analazimika kuhubiri na kuilinda Amani iliyopo nchini kwa nyakati zote kwa maslahi mapana ya vizazi vilivyopo na vinavyokuja.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi waliohudhuria katika Iftari hio Katibu Mtendaji Kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana Zanzibar sheikh Abdalla Talib amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa imani na upendo mkubwa alionao na kuona umuhimu wa kufutari pamoja na watoto yatima jambo linalowapa furaha na kuzidisha upendo kwa viongozi wao.

Sheikh Abdalla amewaomba  watu wengine walio na uwezo kuelekeza nguvu zao kwa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo mayatima ili kupata fadhila kutoka kwa Allah ( S.W ) pamoja na kufikia malengo ya kufunga. 


Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe ..04 / 03 / 2026

Post a Comment

0 Comments