6/recent/ticker-posts

Mhe Hemed apongeza Wazanzibari kuendeleza umoja na mshikamano

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi pamoja na Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba mara baada ya  Iftari aliyowaandalia iliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya kufurahishia Watoto Tibirinzi, Chake Chake Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza umoja na mshikamano baina yao hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. 

Ametoa pongezi hizo wakati akiwashukuru Viongozi na Wananchi  wa Mikoa Miwili ya Pemba mara baada ya Iftar aliyowaandalia iliyofanyika katika Ukumbi wa viwanja vya kufurahishia watoto Tibirinzi Mkoa wa Kusini Pemba. 

Amesema umoja na mshikamano ndio jambo pekee lililosaidia wafanyabiashara kushirikiana kwa pamoja katika kufikia malengo ya Serikali juu ya suala zima la kuwapatia wananchi bei sahihi za bidhaa hasa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan. 

Makaumu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imetoa bei elekezi kwa wafanyabiashara kwa lengo la kuweka usawa na kuwarahisishia wananchi kupata mahitajio yao bila ya usumbufu wowote. 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewatoa hofu Wananchi wa Kisiwani Pemba na Wazanzibari kwa ujumla kwa kusema kuwa Zanzibar inachakula cha kutosha ambacho kinaweza kutumika ndani ya  mwezi mtukufu wa Ramadhani na hata pale utakapomalizika. 

Aidha amewataka Wananchi wa Pemba kuendelea kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini ili kuiwezesha Serikali kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kukifungua kisiwa cha pemba kiuchumi. 

Amesema Amani na mshikamano ndio chemchem ya maendeleo katika Taifa lolote lile duniani hivyo, kila mtu kwa nafasi yake analazimika kuhubiri na kuilinda Amani iliyopo nchini kwa nyakati zote kwa maslahi mapana ya vizazi vilivyopo na vinavyokuja. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mkuu wa Wilaya ya Wete Mhe. ABADALLA RASHID ALI amewapongeza Viongozi wakuu kwa  kuwa mstari wa mbele katika masuala ya kijamii na kiuchumi jambo ambalo linapelekea kuwaweka pamoja wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote. 

Mhe. Abdalla  amesema suala la kuandaa Iftar kwa wananchi ni uthibitisho wa wazi kuwa Viongozi wakuu wana upendo wa hali ya juu kwa wananchi wao na kumpongeza Mhe. Hemed kwa kuendeleza jambo hilo kwa kila mwaka 

Kwa upande wake Mratibu Ofisi ya Mufti Mkuu Pemba Sheikh Said Ahmad amemshukuru Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuwafutarisha waumini na wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba na kumuomba kuuendeleza utamaduni huo kwani huwaweka karibu pamoja na kupata fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhan. 

Amesema suala la kuwafutarisha wananchi kunaendana na hadithi ya Mtume Muhammad ( S.A.W ) iliyosema kumfutarisha mtu aliefunga unapata fadhila sawa na Yule aliefunga, hivyo amewataka waumini kufanya kama vile wanavyofanya Viongozi hao ili kupata fadhila na ujira kutoka kwa ALLAH ( S.W )

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

Leo tarehe ..03 / 03 / 2026


 

Post a Comment

0 Comments