6/recent/ticker-posts

Wizara ya Afya kuimarisha huduma za afya vituo vya afya ngazi ya msingi





Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Ikulu, Saada Mkuya Salum amesema Wizara ya Afya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za afya kwa kupeleka vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika vituo vya afya ngazi ya msingi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa watendaji wa afya wa Wilaya ambapo alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa hivyo ili viweze kuleta tija na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Amefamisha kwa mujibu wa mpango huo, kila kituo cha afya cha kitapatiwa kompyuta mpakato (Laptop) mbili (2) na Tablet moja (1), huku kila Health Center ikipewa Laptop nne (4) na Tablet moja (1) ikiwa na lengo la kuhakikisha vituo vyote vinakuwa na uwezo wa kutumia mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa taarifa za wagonjwa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za afya, pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzinar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema hatua ya kupeleka vifaa hivyo katika vituo vya afya kutasaidia kuimarisha huduma kwa malengo yaliyokusudiwa na kubainisha kuwa serikali imewekeza rasilimali kubwa kwa  kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma bora, za kisasa na zenye viwango vinavyokidhi mahitaji yao.
Amefahamisha kuwa ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya mpango mpana wa mageuzi ya kidijitali katika sekta ya afya Zanzibar, unaolenga kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha uwazi katika utendaji kazi, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi huku Wizara ikipanga mipango yake kwa umakini.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano katika Wizara ya Afya, Mohamed Habib Almafaz, amesema kuwa Wizara inatarajia kupokea kompyuta za mezani (Desktop Computer) 500 ambazo zitagawiwa katika vituo mbalimbali vya afya ili kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya nchini.
Aidha, ameeleza kuwa Wizara imepeleka  kompyuta mpakato (Laptops) 440, Tablets 115, Printers 106 pamoja na UPS 110 ambapo Vifaa hivyo vitasambazwa katika vituo vya afya ngazi ya msingi kwa lengo la kuimarisha ufanisi katika utoaji wa huduma.

 

Post a Comment

0 Comments