Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Jumamosi ya Tarehe 28 Februari 2026, walitiliana saini Hati ya Mashirikiano na Chuo Kikuu cha Warsaw, Poland, katika Mradi wa Utafiti wa Mji Uliozama wa Ras Mkumbuu, Kisiwani Pemba.
Programu hii ya Utafiti itafanywa kwa pamoja na Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari (ZAFIRI) na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Warsaw. Poland, kwa kutumia nyenzo za kisasa za uchoraji ramani wa malikale zilizo ndani ya Bahari kwa kutumia mifumo ya kisasa ua kidijitali.
Utiaji saini huo wa Hati ya Mashirikiano ya Utafiti huu wa pamoja uliratibiwa na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, hapo Vuga, Mji Mkongwe.
Akizungumza katika hafla hiyo fupi ya usaini wa mashirikiano hayo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Dkt Islam Seif, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na jitihada zake za kukuza utafiti wa kisasa wa bahari na malikale unaotumia teknolojia za kidijitali na AI ili kuimarisha Sekta ya Urithi wa Mambo ya Kale Zanzibar katika mukhtadha wa Uchumi wa Buluu.
Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dkt Aboud Suleiman Jumbe alliwashukuru wataalamu wa Akiolojia wa Chuo Kikuu cha Warsaw, kwa utayari wao wa kushirikiana bega kwa bega na Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale na ZAFIRI ili kupata taarifa za kisasa na zenye kujitosheleza katika utayarishaji wa ramani ya chini ya bahari ya Mji huo wa zamani uliozama.
Kwani taarifa hizo hapo zitakapokamilika chini ya Utafiti huu zitawezesha kutoa fursa zaidi kwa Zanzibar kujitangaza kimataifa katika Urithi wa Malikale za Bahari ( Ocean Heritage) na kufungua fursa zaidi za utambuzi wa maeneo zaidi ya kihistoria hapa Zanzibar yenye umuhimu wa kipekee hapa Duniani.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Capt Hamad Bakar Hamad, alisema kuwa utafiti huu wa chininya bahari utatuoa fursa zaidi ya kuzidisha kukusanya taarifa zaidi za utajiri wa Maliasili na Malikale za Baharini na kusaidia katika kuharakisha mipango ya utekelezaji wa Ajenda ya Uchumi wa Buluu.


0 Comments