6/recent/ticker-posts

Siku Mia Moja (100) za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Kipindi cha Pili Awamu ya Nane Utekelezaji wa Ilani ya CCM Mwaka 2025-2030

 

Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, ambae ni Waziri wa Kazi Uwekezaji Zanzibar Mhe.Shariff Ali Shariff  akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Zanzibar, Siku Mia Moja  (100) za Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Kipindi cha Pili awamu  ya Nane, mkutano huo uliyofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Rahaleo Zanzibar. 

Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda ina majukumu ya Kukuza maendeleo ya Viwanda, Kusimamia na kuimarisha mazingira mazuri ya ufanyaji Biashara na Kuhakikisha uwepo wa masoko kwa bidhaa za ndani katika masoko ya Nje ya nchi. Aidha, Wizara katika kutekeleza majukumu hayo inazingatia nyenzo muhimu ambayo ni  Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (C.C.M)  ambapo kwa kipindi cha 2025-2030 na katika awamu ya nane na kipindi cha pili (2) cha siku 100 cha uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wizara  ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imetakiwa kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi  kupitia ibara ya 70  kifungu (i) hadi kifungu (xix) ambapo kifungu hicho kinalenga katika kuimarisha Sekta ya Biashara na ibara ya 71 kifungu (i) hadi (ix) ambapo kifungu hicho kimepanga kuimarisha Sekta ya Viwanda.

Vipaumbele vilivyoanishwa katika ibara ya 70 na 71 katika Sekta ya Biashara na Viwanda vina umuhimu mkubwa katika mipango ya utekelezaji wa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii kwa kuchangia katika mzunguko wa fedha, fursa za ajira na upatikanaji wa bidhaa na huduma.

Ndugu Waandishi wa Habari, Baada ya maelezo hayo mafupi, sasa naomba kuwasilisha utekelezaji wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda katika ilani ya Chama cha Mapinduzi kupitia Sekta ya Viwanda na Biashara katika kipindi cha siku 100 kama ifuatavyo:-

KUIMARIKA KWA SEKTA YA VIWANDA

Ndugu Waandishi wa Habari, Serikali ya awamu ya nane (8) kwa kipindi cha pili inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeweka mkazo maalum katika kuimarisha ukuaji wa Sekta ya Viwanda kama ilivyobainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025-2030.

i. Miongoni mwa Viashiria vinavyotumika kupima maendeleo ya nchi duniani ni ukuaji wa sekta ya Viwanda, ambapo kupitia utekelezaji wa ilani, Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta hiyo kwa kuvutia uwekezaji katika maeneo tengefu ya viwanda hapa nchini kwa uimarishaji wa miundombinu katika eneo la Dunga, Chamanangwe na Pangatupu. Ndugu wanahabari,katika juhudi zake za kuliimarisha eneo Tengefu la Viwanda liliopo Chamanangwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba, mradi wa Maji safi na salama unaojengwa na Kampuni ya “Simba Developer” unaendelea ambapo hadi sasa ujenzi huo umefikia asilima 30.41 kwa hatua za kujenga ukuta unaozunguka tenki, ujenzi wa visima viwili pamoja na ofisi ambazo zinatoa huduma katika eneo hilo. Mradi huo unategemewa kutoa maji kwa Wawekazaji wa Viwanda na wananchi wanaoishi maeneo jirani. 

ii. Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa upande wa eneo la Viwanda Dunga Zuze tayari miradi mikubwa mitatu (3) ya viwanda yenye thamani ya TZS bilioni 203.906 inaendelea kujengwa. Viwanda hivyo ni Kiwanda cha Kuzalisha Dawa za magonjwa ya binaadamu kinachomilikiwa na kampuni ya “Africa Biochem Pharma Co Ltd”, Kiwanda cha nguo “Mama Africa Textile Ltd” na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma (fabricated metal works) “Arines Co. Ltd.” Ndugu Waandishi, Kukamilika kwa miradi hiyo kutazidi kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 20.8 ya sasa na kufikia asilimia 25 mwaka 2030, pamoja na kuchangia upatikanaji wa ajira, kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nje na kuchochea kuimarika biashara nchini.

iii. Ndugu Wanahabari, Wizara kupitia Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa uanzishwaji wa Kiwanda cha Kuchakata Mwani katika eneo la Chamanangwe, Mkoa wa Kusini Pemba. Mradi huu unatekelezwa kupitia mkakati wa Serikali wa kuongeza thamani ya zao la mwani, kuimarisha kipato cha wakulima, kukuza ajira kwa vijana na wanawake, na kuongeza mapato ya Serikali kupitia bidhaa za viwandani zenye ushindani wa Kimataifa. Kwa sasa Kampuni inaendelea na hatua za kununua mitambo ambapo wasambazaji wa mashine hizo tayari wameshalipwa. Mashine hizo zinatarajiwa kuwasili kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kufika Pemba mwisho wa mwezi Machi, 2026 na awamu ya pili inatarajiwa kufika nchini mwezi Juni, 2026. Aidha, Uzalishwaji wa kiwanda hicho unatarajiwa kuwa katika maeneo mawili yakiwemo ya uzalishaji wa chakula cha mifugo (Pelletized Fertilizer) na Uzalishaji wa Mbolea ya Maji (Liquid Bio-Stimulant).

KUIMARISHA MAZINGIRA MAZURI YA UFANYAJI BIASHARA ZANZIBAR.  

Ndugu Waandishi wa Habari, kama tulivyoeleza hapo awali kuwa Wizara ina majukumu ya Kukuza maendeleo ya Viwanda, pia ina jukumu kubwa la kuimarisha Sekta ya Biashara kwa kuimarisha mazingira mazuri ya ufanyaji biashara, utafutaji wa masoko pamoja na urahisishaji wa biashara. Kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi  ya mwaka 2025-2030 kwa kipindi cha siku 100 Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda imefanikiwa kutekeleza shughuli zifuatazo:-

i. Serikali imeendelea kusimamia biashara ya zao la karafuu ambapo Wakulima wa karafuu wameendelea kulipwa TZS 15,000 kwa kilo moja, ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya bei ya soko ya kuuzia nje. Ndugu wanahabari, Idadi ya Wateja wameongezeka na kufikia wateja wakubwa saba (7) kutoka wateja watatu (3) wa awali. Shirika la Biashara (ZSTC) limeuza jumla ya tani 3,702 za karafuu nje ya nchi kwa thamani ya TZS. 59.88 bilioni kwa kipindi cha siku 100 ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kuuza tani 2,827. Aidha, katika jitihada za kuongeza thamani ya ufanyaji biashara Wizara kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) limeweza kuzalisha jumla ya tani 3,423.65 za karafuu  zenye thamani ya TZS. 55.45 bilioni, ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kununua tani za karafuu 2,870.

ii. Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara kupitia Taasisi yake ya Tume ya Ushindani Halali wa Biashara (ZFCC) inaendelea kudhibiti bei elekezi kwa  bidhaa za mchele, unga wa ngano, sukari, mafuta ya kula na saruji; ambapo ndani ya siku 100 za Uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ukaguzi umefanyika kwa kukaguwa jumla ya maduka 375, maghala 18, na Supermarket nne (4) na kubainika kwa Wafanyabiashara tisa (9) walipatikanwa na makosa ya kutoweka bei ya utambulisho katika bidhaa. Wafanyabiashara hao wamechukuliwa hatua pamoja na kupatiwa elimu ya kudhibiti bei za bidhaa zao.

iii. Ndugu Waandishi wa habari, katika kuhakikisha vibali, leseni na ruhusa za kufanya biashara zinatolewa, ndani ya siku 100 za Uongozi wa Dkt. Hussein A. Mwinyi, Wizara imefanya ukaguzi katika maeneo ya biashara 18 na kutoa Hati za usajili wa Biashara 29 kwa Wafanyabiashara, kati ya hizo hati 18 ni mpya na 11 wameongezewa muda. Aidha, Idara ya Biashara na Masoko imeendelea kutoa vibali vya usafirishaji wa mizigo na kufikia vibali 86. Bidhaa zilizosafirishwa kwa kipindi hicho ni bidhaa ya chuma chakavu, mazao ya baharini, Makapi ya ngano na Vitenge/Khanga.

iv. Katika kuendelea na program ya mapitio ya ada na tozo zilizo kero kwa wananchi na wafanyabiashara kwa lengo la kuzifuta, Ndugu Wanahabari, Wizara kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Utoaji Leseni imefanya vikao viwili (2) vya mapitio vya ada na tozo kwa Mamlaka 17 zikiwemo Manispaa, Mabaraza ya Miji, Halmashauri na Mamlaka ya Chakula na Dawa kwa lengo la kuunganisha (harmonization) baadhi ya ada na tozo za Maduka ya Dawa (Pharmacy) ambazo zitapunguza kero kwa Wananchi.

v. Ndugu Waandishi wa Habari, katika kufungua fursa za masoko ya ndani na nje kwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa ndani; Wizara imefanya maonesho ya 12 ya Biashara ambayo yalibeba kauli mbiu ya Kujenga Ukuwaji Jumuishi Kupitia Biashara na Ubunifu”. Maonesho hayo yalikuwa na malengo ya kuitangaza Zanzibar kibiashara; Kuzitafutia masoko bidhaa za wajasiriamali, wafanyabiashara na watoa huduma; Kuwezesha wafanyabiashara wa nchi mbali mbali kukutana na kufahamiana kwa ajili ya kutengeneza mitandao ya kibiashara. Aidha, Katika maonesho hayo jumla ya washiriki walikuwa ni 316 kati ya hao, Taasisi za Serikali ni 101, Taasisi binafsi ni 16, teknolojia 4, wafanyabiashara/wajasiriamali wa ndani 184 na wafanyabiashara 11 kutoka nchi za Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo, Zambia, Msumbiji, Misri na Brazil walishiriki katika maonesho hayo.

vi. Ndugu Wanahabari, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango imo katika matayarisho ya kufanyika kwa Upembuzi Yakinifu (feasibility study) kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha kumbi za mikutano na Maonesho ya Biashara Fumba, ambapo kituo hicho kitakuwa na ukubwa wa hekari 10.7. Ndugu Waandishi wa Habari, katika kuimarisha ukuaji na utafutaji masoko hapa nchini, Kituo hicho kinalenga kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara  katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuunganisha biashara za sekta muhimu za utalii, fedha, mawasiliano miundombinu, elimu, afya na kilimo pamoja na kukuza biashara za ndani na za Kimataifa. Aidha, Mshauri Elekezi kutoka Nchini Korea ambaye anatarajiwa kuanza kazi ya Upembuzi yakinifu   anatarajiwa kufika Zanzibar na kuanza kazi hiyo mwishoni mwa mwezi Februari 2026 na matayarisho ya awali ya kazi hiyo yanaendelea.

vii. Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara imefanya mapitio ya Sheria ya Hakimiliki (Namba 14) ya mwaka 2003 kwa lengo la kuimarisha Usimamizi na Ulinzi wa Hakimiliki pamoja na kufanya Upembuzi Yakinifu “Feasibility Study” ya kuangalia mfumo wake wa uendeshaji na kupendekeza kufanya maboresho ya mfumo wake ili uendane na dhana ya tasnia ya hakimiliki kibiashara. Aidha, katika kuimarisha biashara ya hakimiliki, mirabaha yenye thamani ya TSZ Milioni 90.6 imekusanywa kutoka kwa watumiaji wa kazi za hakimiliki kibiashara na mirabaha hiyo inatarajiwa kugawiwa kwa wasanii wenye hakimiliki.

viii. Ndugu Wanahabari, Wizara imepanga kujenga Maabara za Kisasa ya Upimaji (Testing House) katika eneo la Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa lengo la kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoagizwa na kuzalishwa. Hivi sasa Taasisi ya Viwango (ZBS)inapata changamoto ya kuhifadhi na kushughulikia bidhaa zinazohusiana na ujenzi na chakula zinazowasili kwa wingi kupitia bandari ya Mkoani na Wete. Aidha, ndugu Waandishi, Taasisi inakabiliwa ya kusafirisha   sampuli za bidhaa zikisafirishwa hadi Unguja kwa ajili ya uchambuzi wa maabara. Hali hii husababisha ucheleweshaji mkubwa, ongezeko la gharama, na upotevu wa muda unaoweza kuathiri ubora wa huduma na ufanisi. Kwa sasa Taasisi ya Viwango imeshaandaa Hadidu rejea na BoQ kwa kwa ajili ya ujenzi wa Maabara ya kisasa Chamanangwe Pemba na inatarajia kufanya kazi hiyo kupita bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

ix. Ndugu Waandishi wa Habari, katika kuiwezesha Taasisi ya Viwango kuwa na maabara ya kisasa ili kuwasaidia wazalishaji wa ndani, katika kipindi cha siku 100  Taasisi imewapatia mafunzo wazalishaji wa ndani kwa kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA) kwa ajili ya kuwasaidia kupata alama ya ubora kuthibitisha bidhaa zao wanazozalisha ambapo wazalishaji watatu (3) wamepatiwa Alama ya Ubora ya ZBS baada ya kukamilisha taratibu husika na wajasiriamali wengine tisa (9) wamefanyiwa ukaguzi wa awali na bidhaa zao zinaendelea na utaratibu wa upimaji maabara kwa ajili ya kupatiwa alama ya ubora taratibu zitakapokamilika.

x. Ndugu Wanahabari, Wizara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) imeanzisha Mfumo wa Nyaraka wa “electronic” wa kuhifadhi nyaraka za Usajili wa Biashara na Mali. Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuwekwa miundombinu katika chumba cha kuhifadhi nyaraka na hatua inayoendelea ni kufanyiwa “scan” na kufanyika kwa taratibu za kuingiza nyaraka zote kwenye mfumo huo. Aidha, Ndugu Waandishi wa Habari, Wizara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) imeanza matayarisho ya Mfumo wa Usajili wa Vyombo vya Moto ambao unalenga kuondosha usajili kwa njia ya kawaida (manual) na kupunguza kero kwa Wananchi.

Post a Comment

0 Comments