Na Maelezo Zanzibar 02.03.2026
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha na kusimamia miradi ya maendeleo ya makaazi kwa wananchi wa Zanzibar ili kuwapatia makaazi bora wananchi wake.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe. Rahma Kassim Ali kuhusu siku 100 za Mafanikio ya uongozi wa awamu ya pili ya Dkt. Mwinyi amesema Wizara imefanya mapitio ya Sera na Sheria ya Ardhi ya mwaka 2018 kutokana na mabadiliko ya mahitaji yaliyopo kwa wananchi.
Amesema Wizara imeandaa mpango maalumu wa matumizi ya ardhi katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kujenga mazingira yanayaridhisha kwa lengo la kuweka mandhari na haiba nzuri pamoja na kuondoa ujenzi holela.
“Wizara imekamilisha matayarisho ya awali ya Upangaji na Upimaji katika Kisiwa cha Uzi pamoja na kisiwa cha Kojani Pemba ambapo jumla ya viwanja 142 vimeshapimwa kwa ajili ya makaazi na viwanja viwili (2) vya huduma za kijamii kwa madhumuni ya kutayarisha Mpango wa Matumizi ya Ardhi na kuepukana na ujenzi holela” amefahamisha Mhe. Rahma.
Aidha Waziri Rahma ameeleza kuwa Wizara imeweka eneo la ziada kwa ajili ya viwanda katika eneo la Dunga Zuze (extension) lenye ukubwa wa Hekta 243.96 kwa ili kuchochea uwekezaji wa viwanda nchini kulingana na mahitaji ya uwekezaji.
Hata hivyo, amefahamisha kuwa Wizara inaandaa mpango mkuu wa matumizi ya Ardhi (Master Plan) katika Visiwa vya Unguja na Pemba kutokana na kuwepo kwa uvamizi wa maeneo ya kilimo ambapo kukamilika kwa mpango huo kutasaidia upatikanaji wa maeneo rasmi yatakayotumika kwa shughuli za makaaazi, kilimo, viwanda na huduma nyengine za kijamii.
Kwa upande wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, Waziri Rahma amesema Wizara inaendelea na utaratibu wa usuluhishi wa migogoro kupitia kamati maalum ya usuluhishi ambapo jumla ya migogoro kumi na tano (15) kwa upande wa Unguja na Migogoro 7 kwa upande wa Pemba imepatiwa ufumbuzi.
“Kwa Upande wa utatuzi wa kesi kupitia mahakama ya ardhi za Mikoa, jumla ya kesi mpya mia moja na tano (105) zimefunguliwa Unguja na Pemba ambapo mahakama inaendelea kusikiliza kesi hizo pamoja na za awali ambapo jumla ya kesi mia moja na mbili (102) zimetolewa uamuzi, sawa na wastani wa asilimia 68% ya lengo la kuamua kesi 150 katika kipindi hicho” amefahamisha Waziri huyo.
Amesema Serikali kupitia Shirika la Nyumba inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji mbalimbali wenye nia ya kushirikiana katika uwekezaji wa miradi ya nyumba za makaazi ikiwemo Infinity Group of Company ltd ambae tayari ameanza ujenzi wa nyumba za Kikwajuni (Kwa Mjerumani).
Aidha, Idara ya Maendeleo ya Makaazi imefanya usajili wa umiliki wa fleti ambapo jumla ya fleti 47 zimesajiliwa katika Nyumba za Maendeleo Kilimani, Michenzani na Miradi mipya Mbweni, Paje na Michamvi kwa lengo la kuwapatia umiliki wa nyumba zao ambazo utawawezesha kuanzisha Jumuiya za mashirikiano katika kuendesha huduma mbalimbali katika makaazi yao.
0 Comments