Habari za Punde

RASILIMALI ZA NDANI KUKUZA UCHUMI -- PROF LIPUMBA.

Na Haji Nassor Pemba.

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Wanachi CUF, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, amesema atakapopewa ridhaa kushika nafasi hiyo, atahakikisha anatumia rasilimali za ndani katika kukuza uchumi.

Alisema kuwa zipo rasilimali kadhaa ambazo bado hazijatumiwa na viongozi walioko madarakani, ambapo wamekuwa waking’ang’ania zaidi kutoka nje, jambo ambalo hupoteza haiba na uzuri wa kinachozalishwa.

Lipumba alieleza kuwa pindi zikitumika rasilimali za ndani pia wananchi wenye maisha magumu watafaidika kutokana na wanachokizalisha kununuliwa kwa wingi kutokana na soko la ndani.

Mgombea huyo wa urais wa tiketi ya CUF aliyasema hayo jana huko Masota Shengejuu Jimbo la Kojani ,Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ,wakati alipokua akizungumza na wanachama wa chama hicho katika mkutano wa kampeni.

Lipumba alieleza kuwa wakati umefika rasilimali za ndani kutumika ipasavyo, ili wananchi waliowengi hasa wenye kipato cha chini na wanaozalisha rasilimali hizo kama vile matunda, madini, magogo pamoja na nyengine wawe wanafaidika nayo.

"CUF imebahatika kuwa na mwana-uchumi imara na mwenye sifa hasa za kukuza uchumi wa taifa hili, hivyo kura zenu za ndio ni vyema mkazitia kwa wagombea wote wa CUF ili kutekeleza hilo tena kwa vitendo’’, alieleza Lipumba.

Aidha Profesa Lipumba alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kuhakikisha wanamuweka madarakani mgombe urais wa chama chao Maalim Seif Sharifu Hamad kutokana na kufanya mapinduzi makubwa kwa kushirikiana na rais anaemaliza muda.

Mapema mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa tiketi ya CUF ,Juma Duni Haji alisema kuwa, wagombe wa CUF kwa Zanzibar na Tanzania bara, wanasifa bora zipatazo tano ikiwa ni pamoja na kuwajali wananchi hasa wenye kipacho cha chini.

Nae Makamu Mwenyekiti wa CUF taifa Machano Khamis Ali aliwaomba Wazanzibari na Watanzania kuhakikisha wanawatilia kura za ndio viongozi wote wa chama chao, ili kiweze kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kabla ya hutuba za viongozi hao mgombea huyo wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , aliwapokea wanachama wapya wa CUF 73.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.