Habari za Punde

CUF YAKATAA KUVURUGA UKUSANYAJI MAONI YA KATIBA

CHAMA cha CUF umelitaka gazeti moja la kila siku linalochapishwa jijini Dar es Salaam na mwandishi wake, kukiomba radhi kutokana na kuandika habari za uongo na upotoshaji.

Taarifa iliyotolewa na Chama hicho kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Uenezi na Mahusiano, Salim Bimani zimeeleza kukerwa na gazeti hilo kuandika habari  za uongo.

Mkurugenzi huyo alisema katika gazeti hilo la Jumapili Aprili 10, limedai kuwa vurugu zilizosababishwa kwenye mijadala ya kutoa maoni ya katiba zilifanywa na wafuasi wa chama hicho.

“Taarifa za vyombo hivyo zimekariri zikiarifu umma kuwa wanachama na wafuasi wa CUF ndio waliovuruga mwenendo mzima wa kujadili mswada huo wa mabadiliko ya katiba jambo ambalo si kweli”, ilieleza sehemu ya taarifa ya Bimani.

Alisema hiyo ni taarifa ya uongo, ya upotoshaji iliyotokana na matakwa binafsi ya mwandishi na chombo chake kwa azma ya kukipaka matope chama mbele ya umma.

“Umma wa WanaCUF ni mkubwa, umekerwa kwa kiasi kikubwa cha uongo na upotoshaji huo, hivyo ni wajibu wa chombo husika( na mwandishi wake), kuomba radhi kutokana na taarifa hizo zilizosababisha usumbufu mkubwa kwa jamii”, alisema Bimani.

Aidha alisema habari hiyo imeandikwa kinyume na misingi na mipaka ya Uandishi wa habari na pia ni upotoshaji mbele ya umma.

Chama hicho kimeeleza kuwa kinatarajia kuombwa radhi haraka iwezekanavyo huku watendaji wakitafakari hatua za ziada za kisheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.