Habari za Punde

MAANDALIZI SHEREHE ZA MUUNGANO

Na Mwandishi wetu

MAANDALIZI ya sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 47 ya Muungano wa Tanzania ambayo yatafanyika uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar yamekamilika.

Miongoni mwa maandalizi hayo ni kufanyika ‘rehearsal’ ya gwaride na matumizi ya uwanja huo kwenye siku hiyo ya kilele ambayo ni kesho.

Baadhi ya wageni tayari wamewasili Zanzibar kwa ajili ya kuhudhuria maadhimisho hayo, ambao walifika Zanzibar kwa kuanza kushiriki tamasha la Pasaka, ambalo mwaka huu kitaifa linafanyika Zanzibar.

Wageni wengine wakiwemo wa kitaifa kutoka Mikoa mbali mbali ya Tanzania, wanatarajiwa kuwasili Zanzibar leo kwa ajili ya kushiriki shrehe hizo.

Katika maadhimisho hayo yatakayofanyika asubuhi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Jakaya Mrisho Kikwete, anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi, ambapo atakaguwa gwaride rasmi la Vikosi vya Ulinzi na Usalama lililoandaliwa kwa sherehe hizo.

Miongoni mwa viongozi wa kitaifa watakaohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Baadae vikundi mbali mbali vya utamaduni vitafanya maonesho ili kung’arisha sherehe hizo.

Viwanja vya Amaan vitafunguliwa mapema asubuhi ili kutoa fursa kwa wananchi kuingia kiwanjani na kukaa katika maeneo waliyopangiwa.

Tanzania inaadhimisha miaka 47 kesho kufuatia kuungana kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika tarehe 26 Aprili 1964.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.