MUWAZA inachukua nafasi hii adhiim kutoa pongezi za dhati kwa asasi tofauti za kijamii za Kizanzibari, zikiwemo ZLS, Kituo cha Sheria, Waandishi wa Habari, ZIORI, Jumuia za Kidini na Wazanzibari wote kwa ujumla kwa michango yao madhubuti ya kuitetea Zanzibar kisheria, kikatiba, kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa kupitia Makongamano tofauti ya hivi karibuni.
MUWAZA inatoa HEKO na Shukurani za dhati kwa wote waliotayarisha, walioshiriki na kuchangia katika Makongamano hayo.
MUWAZA vile vile inawavulia kofia Wachangiaji wote pamoja na waliohudhuria katika Mikutano ya Mswada wa marekibisho ya Katiba ya Hoteli ya Bwawani na Skuli ya Haile Selassie, kwa ukakamavu wao, ujasiri wao na ujananchi wao. Haiba ya Zanzibar imetukuzwa upya na MUWAZA inatoa pongezi kwa moyo mkunjufu.
MUWAZA imebaini kwamba lengo zima la MSWADA huo wa Katiba Mpya kama lilivyowasilishwa Zanzibar halikuwa na nia njema kwa Zanzibar
Mfumo wote umeendeleza ile dharau juu ya Rais wa Zanzibar pamoja na Serikali yake ya SMZ kwa kumuweka chini ya Rais wa Tanganyika ambae anaweza kumshauri tu Rais wa Zanzibar pale atakapo au kutomshauri kabisa kama hatataka kufanya hivyo.
Hili halikubaliki kwani suala lolote la Kikatiba lazima lipite kwa makubaliano ya Rais wa Zanzibar ambae anatakiwa awe na haki ya kupiga kura ya VETO kama kutakuwa na jambo la Kikatiba hatakalowafikiana nalo
Utaratibu uliotumika wa kutoshirikishwa kwa SMZ/SUK kikamilifu na ipasavyo nako kunaonyesha dharau ya hali ya juu kabisa kwa mamlaka ya Zanzibar
Mwenendo uliotumiwa na Kamati ya Mswada na wanasheria wa Serikali ya Bara imebainisha kuendeleza tabia ya kutoliheshimu ipasayo BLW na kulitukuza zaidi Bunge la Muungano kwa kupanga kupeleka Mswada huo kwa Spika wa Bunge na hatimae kupitishwa Bungeni bila ya kupanga utaratibu kama huo kuhusu BLW
Kwa wakati huo huo kufichwa kwa Wajumbe wa BLW kuhusu kuja kwa Kamati hiyo Zanzibar ni ukiukwaji usiokubalika kwa Wazanzibari
Kupanga kwa Kamati hiyo ya MSWADA kusikiliza maoni Dar es salaam na Dodoma tu na kulazimishwa katika dakika za mwisho kuamua kuja Zanzibar nako kunadhihirisha dharau kwa Zanzibar
Kutoshirikishwa Ofisi ya kutunga sheria ya Zanzibar itakikanavyo katika utayarishaji wa MSWADA huo na dhamana yote ya usukaji kupewa Wanasheria wa Bara nalo ni tusi kwa kuwa ni dharau na ukiukwaji mwengine wa sheria
MUWAZA imegundua kwamba nia na lengo muhimu la Mswada huo na mchakato mzima wa mjadala wa Katiba Mpya ni kuwa na lengo la kuyabadilisha marekibisho ya Katiba ya Zanzibar ya hivi karibuni yalioitambulisha Zanzibar kama ni nchi, pia kuinyang´anya Serikali ya Zanzibar madaraka yake na vile vile zikiwemo njama za kulivua BLW uwezo na madaraka yake
MUWAZA imetanabahi kwamba mchakato mzima wa kuanzishwa kwa mjadala wa Katiba Mpya haukuwa na nia njema kwa Zanzibar na badala yake ni muendelezo wa mbinu mpya za kuendelea kuitawala Zanzibar
Kwa vile imedhihirishwa kwamba Bunge la Muungano HALINA Mamlaka/Madaraka ya kuanzisha Bunge la kutunga Katiba ya Muungano kwa hivyo MUWAZA inapinga kitendo hicho kwa nguvu zote
MUWAZA inatambua kwamba Katiba Mpya haiwezi kujadiliwa na kubadilishwa kabla mazingira na misingi ya katiba yenyewe hayajabadilishwa kikamilifu hasa kwa upande wa Zanzibar na kutungwa kwa katiba ya Tanganyika.
Wazanzibari wameshuhudia kwamba tatizo sugu linatokana na ukiukwaji wa Katiba ya Muungano wa mara kadhaa tokea mwaka 1964 bila ya idhini na kinyume na maslahi ya Zanzibar.
Kwa vile wanasheria wengi wa ndani na nje pamoja na wadau wengine mbali mbali wameonesha kivitendo kwamba kisheria na kikatiba Muungano haupo kwa hivyo MUWAZA inashauri kwamba pana haja muhimu wa haya yote kutizamwa upya, hii inatokana na ukweli usiopingika kwamba kiini cha tatizo ni Muungano wenyewe na sio kero za Muungano tu. Kwa mfano:-
• Muundo wa kumpora Rais wa Zanzibar Madaraka ya kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais na kuanzishwa kwa cheo bandia cha Mwenza ni kati ya hatua haramu za kuvunja Makubaliano ya Muungano
• Kumgeuza Rais wa Zanzibar kuwa Waziri wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Muungano ni kitendo kingine cha kuvunja Katiba
• Kumshusha hadhi Rais Wa Zanzibar na kumkuza hadhi Rais wa Tanganyika ingawa hawa ni Ma- Rais wa nchi mbili huru katika suala hili la Katiba Mpya ni hatua isiyokubalika kwa Wazanzibari
Kimsingi Katiba ya Muungano imevunja na kukiuka Katiba na Makubaliano ya Muungano kila pale ilipoongeza kipengele ya makubaliano mama 11 ya 1964
Kwa vile Wazanzibari na walimwengu kwa jumla wameshuhudia kinaga ubaga kwamba Wazanzibari wakiwemo baadhi ya Mawaziri wa SMZ/SUK, baadhi ya Wajumbe wa BLW, Wanasheria wa Serikali ya Zanzibar, Wadau wa Kisiasa na wa Asasi za Kiraia mbali mbali wameukataa na kuukana hadharani Mswada huo wa Katiba Mpya, kwa hivyo MUWAZA inapendekeza Mswada huo uondoshwe mezani moja kwa moja, usiwasilishwe Bungeni na kama ukiwasilishwa kimabavu basi Wa-Bunge wote kutoka Zanzibar watoke Bungeni
Kutokana na hali iliyojitokeza na jinsi inavyoendelea MUWAZA inapendekeza yafuatayo:-
• SMZ/SUK ikutane kwa dharura na kwa haraka na itoe msimamo madhubuti usiotetereka wa kuujadili mfumo mzima wa Muungano na kutetea mustakbal wa Zanzibar
• Iinasihi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kurekibisha sheria inayofanya kuzungumzia Muungano ni uhalifu na kupendekeza mabadiliko ya kisheria na ya kikatiba yatakayolinda uhuru na mamlaka ya Zanzibar kimsingi
• Inavishajiisha vyama vya kisiasa, asasi tofauti za kiraia na Wazanzibari wote kwa jumla kulifanyia uchunguzi na utatuzi suala zima la Muungano na kudai haki ya kulipigia kura ya Maoni ambayo itatoa fursa ya kuulizwa Wazanzibari kama Muungano uliopo wanautaka au hawautaki, na kama wanautaka basi iwekwe wazi aina gani ya Muungano huo unaotakikana badala ya huu uliopo wa kizungu mkuti, au wa mshirika mmoja kujifanya kuwa Bwana na mwengine kufanywa kuwa Bibi
• Inalinasihi na kuliomba BLW liitishe mkutano wa dharura haraka iwezekanavyo ili kulijadili kwa kina suala zima la Muungano kabla mjadala mzima wa Katiba Mpya haujaanza
KWA MARA NYENGINE TENA MUWAZA INAUPONGEZA UMMA WOTE WA KIZANZIBARI KWA KUTETEA MUSTAKBAL WA ZANZIBAR
Naomba kuwasilisha kwa heshma na taadhima
Dr. Yussuf Saleh Salim
Mwenyekiti wa MUWAZA
Tunamuomba Mwenyenzi Mungu aibariki Zanzibar pamoja na watu wake.
No comments:
Post a Comment