Habari za Punde

MAALIM SEIF AKARIBISHA WAMISRI KUWEKEZA NCHINI

Na Abdi Shamnah, OMKR

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewaomba wawekezaji kutoka Misri kuja Zanzibar kuwekeza katika sekta mbalimbali ili kuisaidia uimarishaji wa uchumi pamoja na kutoa fursa za ajira kwa vijana.

Maalim Seif alitoa wito huo jana alipofanya mazungumzo maalum na mwaandishi wa habari wa gazeti la ‘Al Masry Al Youm’ la Misri, ambapo pamoja na mambo mengine alitaka kufahamu ushirikiano kati ya Zanzibar na Misri.

Alisema Zanzibar ina eneo dogo la ardhi lenye rotuba ina fursa nyingi za uwekezaji, husa katika sekta za kilimo, uvuvi, mifugo, mawasiliano na utalii, huku ikiwa haina urasimu katika upatikanaji na vibali muhimu kutoka mamlaka zinazosimamia uwekezaji.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea na juhudi za kuimarisha miundombinu ya uwekezaji katika maeneo mbali mbali nchini yakiwemo maeneo huru yalioko Fumba na Micheweni.

Alisema huduma za mawasiliano hususan katika uwanja wa ndege wa Zanzibar, barabara, umeme, maji na simu zimefikia kiwango kinachoridhisha kuvutia wawekezaji pamoja na watalii.

“Tunahitaji makampuni yatakayowekeza katika uvuvi wa bahari kuu, yatakayotumia mbinu bora na vifaa vya kisasa na kuwezesha kujengwa viwanda vidogo vidogo vya kusindika samaki, hapo nchi itanufaika kukuza uchumi, wananchi watapata lishe bora na vijana kupata ajira”, alisema.

Kuhusu sekta ya Utalii, Makamu huyo alisema ni eneo muhimu katika uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar, ambapo umechukua nafasi muhimu baada ya kuanguka kwa zao la karafuu kutokana na kushuka kwa kiwango cha uzalishaji, kuporomoka kwa bei katika soko la dunia.

Aliwaomba wawekezaji wa Misri kuja kwa wingi na kuwekeza katika sekta hizo, kwa kigezo kuwa mbali na kuimarisha uchumi, lakini taifa litaondokana na moja kati ya tatizo kubwa linalokabili la ukosefu wa ajira kwa vijana wake.

Akizungumzia uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema umeiweka Zanzibar katika changamoto kubwa ya kukabiliana na soko ajira pamoja na lile la bidhaa zake.

Mapema Maalim Seif aliwaeleza waandishi hao kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Misri ni wa kihistoria, ulioanza tangu enzi za kupigania uhuru, kutoka kwa waasisi wa nchi hizo Marehemu Gamel Abdel Nasser na hayati Abeid Amani Karume.

Aidha alisema watu wa nchi mbili waliunganishwa kutokana na kufanana kwa tamaduni zao, biashara, kutembeleana na uwepo wa dini ya kiislamu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.