WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameipitisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambayo iliyowasilishwa juzi Barazani hapo na Waziri wa Wizara hiyo Fatma Abdul-habib Ferej.
Bajeti hiyo ilipitishwa baada ya wajumbe wa Baraza hilo kuridhishwa na ufafanuzi wa hoja na masuali yao waliyoyatoa kupata ufafanuzi kutoka kwa waziri huyo.
Akitoa ufafanuzi wa huo Waziri Fatma alisema ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais nje ya nchi zilikuwa na maslahi na faida kubwa kwa maendeleo ya Zanzibar.
Waziri huyo alitaja baadhi ya faida za ziara za Makamu wa Kwanza wa Rais nchi za Mashariki ya Kati ni pamoja na kukutana na wafanyabiashara na wawekezaji ambao baadhi yao wameonesha nia ya
kushirikiana na Zanzibar.
kushirikiana na Zanzibar.
Mbali ya faida hiyo, waziri huyo alisema pia yalifanyika mazungumzo nchini Oman ya kuanzisha Shirika jipya la ndege la Zanzibar, msaada wa uchimbaji mafuta, pamoja na Shirika la ndege la nchi hiyo kuanzisha safari za moja kwa moja visiwani hapa.
Waziri alilazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya Mwakilishi wa Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, kutaka aelezwe faida ya safari hizo ambazo hapo awali hazikuainishwa katika kitabu cha bajeti ya ofisi hiyo.
Aidha waziri huyo alisema mbali ya faida hizo, pia yalifanyika mazungumzo ya kuomba msaada wa ujenzi wa Bandari mpya na kudumisha uhusiano mwema baina ya Zanzibar na nchi za eneo hilo.
Akielezea kwa nini bajeti ya UKIMWI imevimba ikilinganishwa na Idara nyengine, alisema hali hiyo inatokana na kuwepo majukumu mengi na watalaamu sekta hiyo kuhitaji fedha nyingi katika kulishughulikia tatizo la maradhi hayo ambayo yamekuwa janga la jamii.
Alisema sekta za utalii zinapaswa kuwa na mikakati ya kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI, pamoja na kuongeza kasi ya mapambano hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar imekuwa na uingiaji na utokaji mkubwa wa watu.
Alifahamisha kuwa tatizo la maradhi ya UKIMWI limekuwa kubwa na msingi wa kuondoka kwake na kulimaliza kabisa ni mabadiliko ya tabia za watu katika kuachana na mambo yenye kuongeza kasi ya maambukizi.
Akizungumzia juu ya tatizo la dawa za kulevya, waziri huyo alisema Ofisi iko kwenye mikakati ya kuangalia mapungufu ya sheria ili kuweza kuzuia uingiaji wa dawa hizo nchini ambazo zimekuwa zikiathiri vijana ambao ndio nguvu kazi ya uchumi wa Taifa.
Kuhusu uharibifu wa maliasili zisizorekebishwa alilifahamisha baraza hilo kuwa Ofisi yake ipo hatua za mwisho kuweka kanuni ambazo zitasaidia kuzilinda na kuzihifadhi kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya tabia nchi, ikiwemo mashamba kuingia maji ya bahari, maji kuingia chumvi na hata baadhi ya maeneo kumegwa na bahari na kubainisha kuwa Ofisi inaandaa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wakichangia bajeti ya Ofisi hiyo wajumbe hao wajumbe wa Baraza hilo waliomba nyumba za Sober House ambazo zimekuwa zikiwahifadhi vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya kujengwa mbali ya nyuma za makaazi ya watu.
Aidha walisema maradhi ya UKIMWI yamekuwa tatizo kubwa na kusisitiza haja ya kuwepo mabadiliko hasa katika mavazi huku wakitilia mkazo kudumishwa kwa mila na silka za Kizanzibari.
Wawakilishi hao pia walionesha kukerwa na tabia mbaya za uchafuzi wa mazingira hasa ya uchimbaji wa mchanga katika maeneo kadhaa huku sheria za zikikiukwa.
No comments:
Post a Comment