Na Mwanajuma Abdi
BAJETI ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka mpya wa fedha 2011/2012, inatarajiwa kuwasilishwa kesho katika mkutano wa nne wa Baraza la nane la Wawakilishi.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Katibu wa Baraza la Wawakilishi Ibrahim Mzee Ibrahim, huko Chukwani wilaya ya Magharibi Unguja alisema mkutano huo utachukuwa wiki sita ambapo utamaliza mwishoni mwa mwezi Julai.
Alisema usomaji wa bajeti hiyo, utakwenda sambamba na uulizwaji wa masuali 237 na kupatiwa majibu wajumbe wa Baraza, ambapo baada ya kumaliza mchakato wote kutawasilishwa mswada wa sheria ya kuidhinisha matumizi ya serikali kwa mwaka 2011 hadi 2012.
Katibu huyo alisema bajeti ya serikali itawasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, ikiwa ni ya kwanza baada ya kukamilika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka jana.
Aidha katika hatua nyengine Katibu Ibrahim alieleza Baraza la Wawakilishi limeshaagiza janereta kubwa lenye uwezo wa KVA 725, ambalo limegharimu shilingi milioni 335, ambalo litafungwa katika ukumbi huo kabla ya kumaliza kikao cha bajeti ili kuondosha usumbufu wa uahirishwaji wa baraza wakati wa umeme unapozimika.
Alifahamisha kuwa, janereta wanalolitumia kwa sasa ni dogo na linauwezo wa KVA 100, hivyo haliwezi kufanya kazi ipasavyo katika Baraza hilo jipya ambapo la zamani liliweza kufanya kazi.
Katibu Ibrahim alikubali kwamba baadhi ya sehemu ya Baraza hilo lina sehemu zinanyonya maji katika kuta zake jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa alama, kutokana na kasoro hiyo iliyojitokeza katika kipindi cha mvua za masika wameshawasiliana na wataalamu waliojenga jengo hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Hata hivyo, alisema tatizo la ‘eko’ katika ukumbi wa Baraza hilo limeshafanyiwa kazi, hivyo katika kikao hicho wajumbe watasikilizana vizuri.
No comments:
Post a Comment