Habari za Punde

JK AAHIDI KUZITATUA CHANGAMOTO ZA NEC

Na Mwandishi Maalum

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuzitatua changamoto zinazoikabili Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), ili kuiwezesha Tume hiyo kuongeza ufanisi katika utendaji wake.


Changamoto ambazo Rais Kikwete ameahidi kuzitatua za Tume hiyo ni pamoja na ukosefu wa wafanyakazi katika mikoa na majimbo ya uchaguzi, fedha kuendeshea uchaguzi na kucheleweshwa kwa fedha hizo.

Rais Kikwete alitoa ahadi ya kutatua changamoto hizo jana baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Kuhusu changamoto ya kuwa na wafanyakazi katika mikoa na majimbo, Rais Kikwete alisema ni utambuzi mzuri. “Naliafiki. Tengenezeni utaratibu mzuri wa kuweza kulifanikisha. Najua litaongeza gharama lakini litaongeza ufanisi katika kuendesha chaguzi zetu vizuri zaidi.”

Akizungumzia kutokupata fedha za kutosha na fedha hizo kutolewa zimechelewa, Rais Kikwete aliahidi serikali itahakikisha kuwa kiasi cha sh. 2.7 bilioni ambacho ni deni kwa Tume kutokana na shughuli za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, zinalipwa haraka.

Rais Kikwete aliipongeza Tume hiyo kwa kuandaa, kuendesha na kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambako Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipata ushindi na hatimaye kuunda serikali.

Wakati huo huo, Rais Kikwete jana alikutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland, Eamon Gilmore ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa nchi hiyo.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, viongozi hao wawili walijadili masuala mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa na masuala yanayohusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Waziri Gilmore ambaye aliwasili nchini juzi  atazuru Tanzania kwa siku nne na miongoni mwa mambo atakayoyafanya ni kutembelea miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Jamhuri ya Ireland na kukutana na viongozi mbalimbali wa Tanzania.

Tanzania na Jamhuri ya Ireland zimekuwa na uhusiano wa miaka mingi na Ireland imekuwa inasaidia miradi ya elimu, afya, kilimo, utawala bora na juhudi za kupunguza umasikini katika Tanzania kupitia MKUKUTA.

Rais Kikwete alimueleza kuhusu visheni 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulitangazwa mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii.

Waziri Gilmore alipongeza uhusiano mzuri na wa miaka mingi kati ya nchi hizo mbili na kuahidi kuwa serikali yake itaendelea kuyatia moyo makampuni, taasisi na wakala kutoka Ireland kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.