Ataka Airport Zanzibar ifanye kazi saa 24
Na Abdi Shamnah, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka watendaji wa vikosi vya Ulinzi na Usalama Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Zanzibar, kuachana na vitendo vya kuwabughudhi na kuwaomba wageni, kwani vinalitia aibu Taifa.
Alisema kuna tabia iliyojengeka miongoni mwa watendaji wa vyombo hivyo vya kuwabughudhi na kuwanyanyasa wageni wanapoingia na kutoka nchini, na wengine kuomba omba.
Maalim Seif amesema hayo jana ukumbi wa VIP wa uwanja wa Kimataifa wa Karume, baada ya kupokea taarifa ya shughuli za uendeshaji wa uwanja huo na kupata fursa ya kuyatembelea maeneo kadhaa na hatimae kutoa maelezo kuhusiana na changamoto mbali mbali zinazoikabili Mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar.
Kufuatia kadhia hiyo ameutaka uongozi wa vyombo vinavyohusika kuwaondosha mara moja watendaji wote wenye tabia hizo, ambao kwa upande mwengine alisema ni chimbuko la kuvujisha mapato ya Serikali.
Alifafanua kuwa idara ya uhamiaji ndio chombo chenye mamlaka ya kushughulikia wageni wanaoingia na kutoka nchini, hivyo kushangazwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa vyombo vyengine kuanza kuwasumbua wageni wakati wakiwa tayari wameshatoka nje ya geti la uwanja.
Aliagiza kuwepo ushirikiano wa karibu na chombo hicho pale panapokuwepo mashaka juu ya mgeni aliekuwa ndani ya ndege.
Alisema inashangaza kumuona mfanyakazi wa kiwanja hicho akiwa ndie mpokeaji wa ‘Briefcase’ ya mgeni, hatua aliyoeleza inathibitisha kwa kiasi gani wafanyakazi hao walivyojikita katika ulaji rushwa.
Alisema mazingira yanayoonesha kuwa waingizaji wa dawa za kulevya wana ushirikiano wa karibu na baadhi ya wafanyakazi kiwanjani hapo, ambao huambulia kiasi kidogo cha fedha na kuacha kuzingatia athari zinazoikabili jamii.
Katika hatua nyingine Maalim Seif aliitaka Menejiment ya Uwanja huo kuondoa muhali na kuwaondosha mara moja watendaji wote wasiofuata kanuni na taratibu za utendaji kazi na kupelekea kuvuja kwa mapato.
Alisema mbali na idara hiyo kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni saba kwa mwaka, kiasi hicho ni kidogo mno na kuonyesha mashaka makubwa ya kuwepo mianya ya kuvuja kwa mapato kupitia kwa watendaji wasio waaminifu,
Akigusia juu ya ushughulikiaji wa huduma za mizigo katika uwanja huo, Maalim Seif alimtaka Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, kuangalia kwa makini na kuhakikisha Kampuni iliyopewa kazi ya kushughulikia mizigo inafanyakazi zake kwa mujibu wa mikataba iliyowekwa.
Alimtaka Waziri huyo kuondoa muhali na kukaa na mmiliki wa Kampuni hiyo (aliyepewa mkataba wa miaka 30), huku akihoji juu ya utoaji wa huduma dhaifu uwanjani hapo.
Alisema anashangazwa katika karne hii ya 21, wakati uwanja wa Ndege wa Zanzibar, ukinadiwa kuwa wa Kimataifa, mizigo imekuwa ikibebwa na kutoendeshwa kwa mkanda kama ilivyo katika viwanja vyengine vyote duniani.
Akitoa maelezo juu ya baadhi ya changamoto zinazoikabili mamlaka hiyo, Maalim Seif aliitaka Menejiment kujiimarisha zaidi ili kuweza kutoa huduma kwa saa 24.
Alisema katika kipindi kifupi kijacho kuna matarajio ya kupata idadi kubwa ya wasafiri (watalii) kupitia mashirika mbali mbali ya Ndege duniani, ikiwemo yatakayoleta ndege zake usiku, hivyo aliagiza kuimarishwa kwa huduma za taa.
Aidha aliitaka menejment hiyo kusimamia vyema miradi inayoendeshwa kiwanjani hapo kwa kuchagua kampuni zenye uwezo na sifa bora za ujenzi pamoja na kutaka kuondokana na tabia ya kuzitetea kampuni kwa ajili ya maslahi binafsi.
Vile vile alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili kufahamu umuhimu wa usalama wa uwanja huo na kuacha kufanya uharibifu, kuingia katika maeneo yasiyoruhusiwa au kuvamia maeneo ya ardhi.
Alitaka sheria zilizopo (Regulations) zitangazwe na kusimamiwa ipasavyo, ikiwa pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuzikiuka.
Aidha aliutaka uongozi huo kukaa pamoja na mkandarasi wa ujenzi wa uzio ili kuhakikisha unamalizika katika kipindi kifupi kijacho, na kutoa hakikisho la usalama kwa ndege zinazotua.
Juu ya hoja ya kuwepo mwekezaji mwenye azma ya kuendesha menejiment ya uwanja huo, Maalim Seif alikiri na kusema sera ya Serikali inalenga viwanja vyote vya ndege kuendeshwa na Wazanzibari wenyewe, lakini pia inazingatia ushindani uliopo kati yake na majirani zake.
Akito mifano ya nchi za Kenya na Dubai, alisema menejiment zake zinaendeshwa na wageni na kuainisha faida iliopo katika utoaji wa huduma bora pamoja na kutoa elimu kwa wazalendo, ili pale wageni hao wanapoondoka nafasi hizo zinarudi mikononi mwa wazalendo wenyewe.
Alisema kuna wawekezaji walioomba kuendesha uwanja huo kwa ubia, hali itakayoleta ushindani wa kibiashara, ikizingatiwa uwanja huo ndio unaoongoza kwa kuwa na njia refu zaidi ya kurukia ndege katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo, Maalim Seif alipata fursa kutembelea maeneo kadhaa ikiwemo eneo linalotumiwa na watu mashuhuri na viongozi wakuu (V.I.P), kituo cha Zimamoto, eneo la kuhifadhia mizigo, Ofisi za Oman Air, kuangalia uzio pamoja na ujenzi wa jengo jipya la kisasa la kufikia abiria.
No comments:
Post a Comment