Habari za Punde

WAJASIRIAMALI 16 KUSINI WAFAIDIKA NA RUZUKU

Na Mwanajuma Abdi

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kuishajiisha sekta binafsi katika harakati za kukuza uchumi wa nchi, badala ya kufanyakazi hiyo peke yake.


Mkurugenzi Mratibu wa Program za Uwezesjaji Wananchi, Kiuchumi na Ushirika, Ameir Haji Sheha, alisema hayo katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa wajasiriamali wa Fanikiwa Kibiashara (BDG) wa Mkoa wa Kusini Unguja, iliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar, Chwaka.

Alisema uchumi wa nchi hauwezi kukuzwa na serikali pekee bali sekta binafsi nayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, ambapo mradi wa wajasiriamali Fanikiwa Kibiashara umewashirikisha moja kwa moja wajasiriamali wadogo wadogo kwa ajili ya kukuza vipato na kuondokana na umasikini.

Alisema jitihada mbali mbali zinachukuliwa na Wizara hiyo, katika kukuza uzalishaji ili uchangie uchumi wa nchi, ambapo changamoto kubwa ipo kwa wajasiriamali hao 16 waliofaulu, na kukabidhiwa ruzuku kwa ajili ya kuendeleza miradi ya biashara zao.

Nae Ofisa wa Tawala ya Mkoa wa Kusini Unguja, Sabri Abdallah ambae alimuakilisha Mkuu wa Mkoa huo, alisema ruzuku walizokabidhiwa wajasiriamali hao zina lengo za kuwapatia stadi za uzalishaji katika miradi waliyoianzisha, ambapo baadae wataweza kukopesheka katika benki zilizopo nchini.

Alifahamisha kuwa, zawadi hiyo ambazo kila mmoja alikabidhiwa hundi ya shilingi 1,100,000 baada ya kumaliza mzunguko wa tatu wa mafunzo ya BDG, yaliyoanza mwaka 2009 chini ya taasisi tatu ya Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCCIA).

Meneja wa Uhusiano wa Biashara wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Mohammed Nuhu alisisitiza kwamba, alieleza kuingia katika mradi wa BDG ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo ili waimarishe zaidi kwa ajili ya kuweza kukopesheka katika mabenki.

Aliahidi kuwa PBZ ipo pamoja na wajasiriamali hao kwa lengo la kukuza uchumi na kuondosha umasikini kwa wananchi wa Zanzibar.

Nae Mwakilishi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha, alisema mafunzo waliyowapatia wajarisiamali hao yatawasaidia katika kuwaoa mbinu za kibiashara, utafutaji wa masoko na usajili, ambapo lengo ni kuunga na Serikali katika kuwawezesha wananchi.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na wakulima (ZNCCIA), Awadhi Ali Said aliwahimiza wajasiriamali hao waliopata mafunzo wayatumie vizuri katika kuendeleza biashara endelevu pamoja na kujituma zaidi kwani sekta binafsi inamchango mkubwa wa uchumi wa nchi.

Mradi wa BDG umeanza miaka miwili iliyopita, ambapo mwaka 2009, walipatiwa mafunzo wajasiriamali 123, mwaka 2010 wajasiriamali 190 nwa mwaka huu wamepatikwa 205 Unguja na Pemba, ambapo 16 katika Mkoa wa Kusini wamefaulu vizuri na kukabidhiwa zawadi na Afisa Tawala wa Mkoa wa Kusini Unguja, Sabri Abdalla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.