Habari za Punde

ABIRIA MV SERENGETI WANUSURIKA KUFA

Yawasili Mkoani kwa injini moja baada ya nyengine kufeli

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ABIRIA waliokuwa wakisafiri kwa meli ya MV Serengeti usiku wa kuamkia jana wakitokea Zanzibar kwenda Pemba, wamenusurika kufa baada ya injini moja ya meli hiyo kushindwa kufanya kazi ikiwa safarini.

Taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), zimefahamisha kuwa, meli hiyo iliyosajiliwa Zanzibar iliondoka bandarini huko mnamo saa 3:00 usiku wa juzi ikiwa na abiria wapatao 810 pamoja na mizigo.

Imefahamika kuwa, ikiwa njiani, injini moja ya meli hiyo ilipata hitilafu na kushindwa kuendelea kufanya kazi.

Kutokana na hali hiyo, vikosi vya ulinzi na uokozi viliandaliwa ili kukabiliana na dharura yoyote ambayo ingeweza kutokea kufuatia hitilafu hiyo.

Hata hivyo, taarifa ya SUMATRA ilisema, kwa mwendo mdogo, meli hiyo iliweza kuendelea na safari kwa kutumia injini moja na kuwasili katika bandari ya Mkoani kisiwani Pemba mnamo saa 4:35 asubuhi, badala ya saa 12 jana Julai 15, 2011, ikiwa imechelewa kwa takriban saa tano.

Abiria wote waliokuwemo katika meli hiyo pamoja na mabaharia, walishuka bandarini hapo salama usalimini.

Katika siku za hivi karibuni, kumeripotiwa malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wasafiri wa meli zinazokwenda kati ya Pemba na Unguja, kwamba zimekuwa mbovu na kutaka mamlaka husika zizidhibiti.

Katika tukio la hivi karibuni, meli uya Burak ambayo pia ilikuwa ikitokeac Zanzibar kwenda Pemba, ilijikuta ikitia nanga katika bandari ya Tanga kutokana na upepo mkali wa Kusi unaoendelea kuvuma nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.