Habari za Punde

ELIMU YA MSINGI KUUNGANISHWA KWENYE MTANDAO - WAZIRI

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kushirikiana na serikali ya Marekani itatekeleza mradi mkubwa wa elimu ya msingi Zanzibar kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano.

 Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban ameyasema hayo hapo jana jioni wakati alipokuwa akiwasilisha bajeti ya Wizara yake katika ukumbi wa baraza la Wawakilishi mbweni Zanzibar.
 Amesema teknolojia hiyo itasaidia sana katika kuimarisha ufundishaji wa elimu ya msingi nchini.
 Waziri Shaaban amesema kuwa skuli zote za msingi za Unguja na Pemba zitafaidika kwa kupatiwa kompyuta zitakazounganishwa na mtandao wa internet kwa lengo la kurahisisha elimu hiyo.
 Akizungumza juu ya suala la bodi ya mikopo ya elimu ya juu zanzibar waziri huyo amesema, bodi ya mikopo ya elimu ya juu zanzibar itaanza kufanya kazi zake rasmi mara tu taratibu za kisheria zitakapokamilika.
 Aidha jumla ya wanafunzi 250 wanatarajiwa kudhaminiwa na bodi hiyo kwa kipindi cha fedha cha mwaka 2011/2012.
 Waziri Shaaban amesema kuwa katika mwaka ujao wa fedha wizara yake imepanga kutekeleza jumla ya miradi tisa ya maendeleo ambapo kati ya hiyo miradi minne itatekelezwa kwa mashirikiano ya kati ya serikali na washirika mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi.
 Kikao hicho leo kinajadili hotuba hiyo baada ya hapo jana kuahirishwa baada ya kusomwa hotuba ya wizara hiyo na hotuba ya Mwenyekiti wa kamati ya baraza la Wawakilishi wa Wizara hiyo.
 Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.