Habari za Punde

MAALIM SEIF ZIARANI PEMBA KUIMARISHA CHAMA CHA CUF

Na Abdi Shamnah

 MAKAMU  wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewahakikishia wananchi kisiwani Pemba kuwa Serikali inafanya kila juhudi kuimarisha uchumi wake na kuvutia wawekezaji, ili kubadili hali  zao za maisha kuwa bora.


 Maalim Seif ambae pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amesema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati alipozungumza na wananchi wa Majimbo ya Ziwani pamoja na Wawi, ikiwa ni mtiririko wa ziara zake za kuimarisha chama cha CUF kupitia Operesheni Zinduka namba 2, kazi inayokwenda sambamba na mikutano na wananchi.

 Alisema viongozi wa Serikali ya Zanzibar, ilio chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wanafanya kazi kwa mashirikiano makubwa , bila ya kuzingatia itikadi za vyama vyao, hatua aliyosema imeongeza kasi ya kufikia maendeleo makubwa na ya haraka.

 Aliwaeleza wananchi hao kuwa  Serikali inafahamu kwa kina tatizo la upandaji wa bidhaa mbali mbali muhimu linalowakabili wananchi na kuainisha hatua zinazochukuliwa na Serikali, na kusema mkazo zaidi umeelekezwa kuongeza uzalishaji wa chakula, hususan mchele kupitia kilimo cha umwagiliaji maji.

 Alisema mabadiliko yalioikumba Dunia yaliotokana na majanga mbali mbali yakiwemo  ya kimaumbile, yamesababisha kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa muhimu, huku mahitaji yakiongezeka, hali iliyoiweka  Zanzibar  ikiwa haina njia ya kujinasua.

 Alisema mbali na Serikali kujikita katika kilimo cha umwagiliaji maji kwa msaada wa wahisani, lakini pia kuna haja kwa wananchi kufanya juhudi katika uendelezaji wa kilimo cha mpunga cha kutumia mvua, na kutoa rai ya kuitumia vilivyo mbegu bora ya NORICA iliofanyiwa utafiti wa kutosha.

 Aidha alisema Serikali inakusudia kufidia gharama za pembejeo, mbolea, dawa za magudu na wadudu pamoja na kuwashajiisha mabwana shamba kuwa karibu na wakulima, ili kutoa msukumo katika kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Maalim Seif alisema katika dhana ya kuondoa umasikini na kuwapatia ajira vijana, Serikali inalenga kupanua wigo wa uwekezaji katika sekta za uvuvi wa bahari kuu pamoja na ufugaji.

 Alisema kuna kampuni kadhaa zilizoonyesha nia ya kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu, ikiwemo ile inayolenga kujenga kiwanda cha usindikaji wa samaki kisiwani Pemba na nyingine kujenga kiwanda kwa ajili ya ujenzi wa boti ndogo zitakazosaidia wavuvi wazalendo kuendeleza uvuvi katika maeneo ya pwani.

 Alisema pia imejitokeza Kampuni ilionyesha azma ya kujenga kiwanda cha usindikikaji wa nyama  kisiwani Unguja na hatimae kuuza ndani na nje ya visiwa hivyo.

Alifafanua kuwa mbali na Serikali kupata mapato makubwa kupitia wawekezaji hao lakini miradi hiyo itaweza kutoa ajira kwa kiwango kikubwa cha vijana wa Kizanzibari.

Akizungumzia azma ya Serikali katika upanuzi wa viwanja vya ndege Unguja  na Pemba,  sambamba na ujenzi wa Bandari ay mizigo itakayotoka eneo la Mpiga Duri hadi Beit el ras, pamoja na utengenezaji wa bandari za Mkoani na Wete, inalenga kuimarisha upatikanaji wa ajira na kuirejeshea hadhi yake Zanzibar kama kituo muhimu cha biashara Afrika Mashariki.

 Alisema  Serikali inaendeleza miradi hiyo kwa kuzingatia uwiano wa kimaendeleo kati ya visiwa vya Unguja na Pemba na kuepuka kisiwa kimoja kuachwa nyuma.

 Katika hatua nyingine Maalim Seif aliwataka wananchi hao kushirikiana na Serikali katika juhudi zake za kuwaondolea umasikini, kwa kuwafichua watu wote wanaofanya uharibifu wa kukata mikarafuu pamoja na wasafirishaji wa magendo ya zao hilo.

 Aliwaeleza wananchi hao kuwa fedha zinazotokana na mauzo ya karafuu ndio zinazotumika katika ununuzi wa madawa hospitalini, madawati, ujenzi wa maskuli pamoja na mambo mengine ya maendeleo, hivyo aliwataka kutangaza vita dhidi ya wafanya magendo wote .

 Alisema Serikali inaendelea na mchakato wa kuwatambua watu wote pamoja na viongozi wa Serikali wanaojishughulisha na kazi za magendo kwa kupitia kijiji hadi kijiji, na kuahidi hatua kali za kisheria kuchukuliwa kwa yeyote atakaepatikana akijihusisha na makosa hayo.

 Alisema Serikali imefanya maamuzi magumu ya kutoa asilimia 80 ya fedha zinazotokana na mauzo ya zao hilo kutoka soko la Dunia, ili zirudi kwa wakulima wenyewe na asilimia 20 iliobaki kwenda ZSTC kwa ajili ya uimarishaji na  ustawi wa zao hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.