Habari za Punde

MAJIBU KWA LULA WANDALI

WANAOTAKA MUUNGANO UVUNJIKE WATOKE BUNGENI

Muungano wa Tanzania kimsingi,ulivunjwa rasmi April 1964, na yule yule muasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Na Laila Abdulla

Naelewa utashangaa kusikia hivyo. Mara tu baada ya kuapishwa Mwalimu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na baadae kujulikana kama Tanzania kwa mujibu wa kitabu cha Rais Mstaafu Aboud Jumbe wa Zanzibar, "THE PARTNER-SHIP", ni kuifuta Tanganyika katika ramani ya dunia. Hii ilimshangaza Jumbe.

Kwa kuifuta Tanganyika, Zanzibar, kimsingi, haikuwa na mshirika tena katika Muungano. Kwani, katika ndoa akifariki mmoja kati ya mume na mke, ndoa huwa imekwisha na yeyote kati yao aweza kubaki pekee au kufunga ndoa mpya.

Kilichosalia Bw.Lula ni kuutambua tu urithi aliotuachia Marehemu Mwalimu Julius Nyerere siku ile alipotawazwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kilichofuatia baada ya hapo ni mazingaombwe au niyaite "Abrakadabra." Kwani utaunganishaje nchi mbili ikiwa moja haipo?

Sasa swali linakuja Zanzibar imeungana na nani tangu April 26,1964?. Haikuungana na Tanzania, kwani, kabla ya tarehe hiyo, haikuwapo nchi au dola iliyoitwa hivyo. Kwa hivyo bila ya Tanganyika, hakuna MUUNGANO. Na kwa kuwa hakuna kitu kinachoitwa Muungano, basi hakuna tena KERO za Muungano.

Kilichobaki ni tatizo la Zanzibar na wazanzibari wenyewe. Kutojitangaza ilivyo na walivyokuwa, tangu sheria ya April 26 1964 ya kuizika Tanganyika, wao wamebaki vile vile walivyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Peoples Republic of Zanzibar , kisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sasa Serikali ya umoja wa kitaifa.

Lakini nani atathubutu kwenda Baraza la wawakilishi Chukwani au Redio Zanzibar, Rahaleo na kunadi kuwa, "Kuanzia leo bila ya kuwapo Tanganyika, Zanzibar ni nchi huru na si sehemu ya Tanzania?."

Kiongozi wa Zanzibar shupavu wa kunadi hivyo angelikuwa mtu kama Marehemu muasisi wa pili wa Muungano huo - Mzee Abeid Amani Karume ambae aliwahi kunukuliwa akisema: 'Muungano ni kama koti tu likikubana unalivua'.

Wengine wenye ujasiri wa aina hiyo upande wa Tanganyika ni mtu kama Kasisi Christopher Mtikila na upande wa Zanzibar, Imam Farid aliyeuchana ule mswada wa mageuzi ya Katiba hadharani. Lakini wote hao wawili, ni Viongozi wa dini ambao wanajaribu kucheza dimba la siasa pia.

Kwa hivyo Bw Lula nihitimishie kwa kusema, Zanzibar ni ya Wazanzibari na wanamuhitaji kiongozi shupavu na jasiri atakaeweza kumfunga PAKA kengele kuhusu ukweli huo wa Muungano wetu. Wananchi tayari wamekwisha amka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.