Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetilia saini na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mkataba wa msaada wa kuwajengea uwezo watendaji wa SMZ utaogharimu zaidi ya dola za Marekani 507,000.
Utiaji saini huo umefanyika jana, katika ukumbi wa wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, ambapo Waziri wa Wizara hiyo, Omar Yusssuf Mzee aliiwakilisha SMZ na Serikali ya China imewakilishwa na Balozi Mdogo wa China aliyopo Zanzibar, Chen Qinman.
Waziri Omar alisema msaada huo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kimafunzo watendaji wa Serikali, ambapo watakwenda nchini China kwa awamu tofauti kuanzia mwezi Augosti, Novemba na kundi la mwisho Februari mwakani.
Alieleza mafunzo hayo yatayochukuwa karibu siku tisa hadi 10 nchini China yatawajumuisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa SMZ, Wenyeviti wa Kamati wa Baraza la Wawakilishi, baadhi ya wakuu wa wilaya, baadhi ya watendaji wa Halmashauri na maofisa Wadhamini.
Alifahamisha kuwa, programu za mafunzo hayo yatajumuisha mapinduzi ya uvuvi, ambao utajumuisha mafunzo katika ufugaji wa samaki baharini, ufugaji wa chanza, kamba, kilimo cha umwagiliaji maji, elimu na miundombinu na mawasiliano.
Nao Balozi Mdogo wa China, aliyekuwepo Zanzibar alisema wamekuwa na uhusaino wa muda mrefu katika nyanja mbali mbali katika kasi ya kukuza uchumi wa nchi.
Alieleza mwaka jana, China iliwapeleka katika mafunzo Wazanzibari 50, ambapo mwaka huu watawapeleka zaidi ya 200 ili kujifunza masuala mbali mbali hususani katika kilimo, uvuvi, elimu na mawasiliano.
Katika hatua nyengine Balozi Chen alimueleza Waziri Omar kwamba China inakusudia kuijenga upya ICU ya hospitali kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kuwapatia madaktari mafunzo kwa ajili ya kuiendesha, sambamba na kuleta vifaa ili iweze kufafanana na za kimataifa.
Nae Waziri Omar alishukuru kwa hatua hiyo Serikali ya China kutaka kuleta wataalamu wake ili waje kufanya tathmini katika ICU na baadae kujengwa upya, ambapo aliwataka wananchi kuwa wastahamilivu maendeleo makubwa yatafanyika nchini katika huduma za kiafya na kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
No comments:
Post a Comment