KAMATI Maluum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Zanzibar, imewateuwa wajumbe wapya wa sekretarieti ya Kamati hiyo pamoja na kupitia majina 21 ya UVCCM wanaowania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, oOisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Issa Haji Ussi, amesema wajumbe hao wameteuliwa baada ya kufanyika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Jumapili Ofisi hiyo mjini hapa, chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.
Alisema walioteuliwa kushika nyadhifa za wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar ambao wataongoza katika Idara mbali mbali ni Machano Othman Said ameteuliwa kuwa katibu Kamati Maalum ya NEC- Organaizesheni, ambapo awali alikuwa ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) nafasi ambayo kwa sasa itashikiliwa na Haroun Ali Suleiman.
Alieleza wajumbe wengine walioteuliwa ni Issa Haji Ussi atakuwa ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC- Itikadi na Uenezi, ambapo nafasi hiyo awali ilikuwa ikishikiliwa na Vuai Ali Vuai ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na Mansoor Yussuf Himid ataendelea kuwa Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Uchumi na Fedha kwa chama hicho.
Aidha aliongeza, kikao hicho kilijadili majina 21 ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) waliojitokeza kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja huo, ambapo mapendekezo ya kamati hiyo yametolewa.
"Jumla ya wanachama 21 wa UVCCM wamejitokeza kuomba kugombea nafasi hiyo kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Hamad Masauni Yussuf mnamo Mei 18, mwaka jana", alisema Issa.
Alifafanua kuwa, kati ya majina hayo 19 ni vijana kutoka Zanzibar na wawili kutoka Tanzania Bara, ambapo alisisitiza kwa mujibu wa utaratibu na kanuni za UVCCM kwamba Makamu Mwenyekiti akitokea Tanzania, lazima Mwenyekiti awe Mzanzibari hivyo majina hayo mawili yatakuwa hayawezi kufuzu katika mchujo hapo baadae.
Alisema tayari kanuni zishawekwa haziwezi kuvunjwa, ambapo wagombea hao wawili wa Tanzania Bara wametumia haki yao ya kidemokrasia lakini wamekiuka kanuni.
Hata hivyo, Issa alikanusha kuchukuwa fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM, ambapo alisisitiza kwa waandishi waamini kauli yake na sio kusikia maneno pembeni.
Alieleza kwamba, CCM ni chama kikubwa chenye wanachama wengi, kimbilio la wanyonge, kinaheshimika na kinafuata misingi ya kidemokrasia, ambapo alihahakisha ushindi mkubwa wa kishindo utapatikana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema Kamati Maalum ilimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010-2015, pamoja na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi kuanza kuzitekeleza kwa vitendo.
Aliendelea kusema, hatua zinazochukuliwa na Dk. Shein zina lengo la kuinua hali za wananchi wa Unguja na Pemba za kuwapunguzia mzigo wa maisha ili kufanikisha lengo la kupunguza umasikini, ambapo miongoni mwa hatua hizo ni kuongeza mishahara ya watumishi wa Serikali kwa asilimia 25, kupandisha bei ya karafuu kutoka shilingi 5,000 hadi shilingi 10,000 kwa kilo moja ya daraja la kwanza na shilingi 9,500 kwa daraja la pili.
Issa alifahamisha kuwa, Serikali imeelekeza nguvu katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutumia kauli mbiu ya 'Mapinduzi ya kilimo' kwa kupunguza bei ya pembejeo za kilimo na gharama za matrekta, ambapo kwa polo moja la mbolea ya TSP itauzwa kwa shilingi 16,000 badala ya shilingi 32,000 na mbolea ya UREA ni shilingi 10,000 badala ya 20,000, punguzo hili ni la asilimia 50 pamoja na mbegu ya mpunga itauzwa kwa shilingi 10,000 kwa kilo badala ya shilingi 25,000.
Hata hivyo, alieleza Serikali imepunguza kwa asilimia 75 bei ya kuchimbua na kuburuga mashamba kwa kutumia trekta kutoka shilingi 32,000 kwa eka hapo mwanzo na sasa ni shilingi 16,000 kwa eka, sambamba na kupunguzwa kwa bei ya dawa ya kuua magugu kutoka shilingi 12,500 kwa lita hadi shilingi 6,000 ikiwa ni punguzo la asilimia 52.
Alisema kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Zanzibar imeridhiswa na hatua zilizofikiwa na Serikali, ikiwemo utekelezaji wa vitendo wa ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Dira ya maendeleo ya 2020 na mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar wa mwaka 2010-2015 (MKUZA II).
No comments:
Post a Comment