TIMU ya taifa ya mchezo wa judo Zanzibar, imerejea nchini jana baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki mwaka huu yaliyofanyika katika hoteli ya Landmark mjini Dar es Salaam Julai 17 na 18, 2011.
Katika michuano hiyo ya tano, Zanzibar ilimudu kuzoa medali 11, zikiwemo sita za dhahabu na tano za fedha ikiwa haijatwaa shaba yoyote na kuibuka mshindi wa kwanza kati ya nchi nne zilizoshirki ngarambe hizo.
Mbali na medali hizo, timu hiyo pia ilikabidhiwa kikombe cha ushindi wa jumla wa mashindano hayo ambayo pia Tanzania inayatumia kupata wachezaji watakaoiwakilisha katika mashindano ya bara la Afrika (All Africa Games) yatakayofanyika nchini Msumbiji mwezi Septemba.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Kenya iliyonyakua medali kumi (dhahabu 1, fedha 4, shaba 5), Burundi ikafuatia katika nafasi ya tatu kwa kutia mikononi medali saba (dhahabu 1, fedha 1, shaba 5) na Tanzania Bara ikashika mkia na medali tano (dhahabu 1, shaba 4).
Walioiletea medali za dhahabu Zanzibar kwa upande wa wanaume katika uzito tafauti ni Hassan Hussein Khamis, Mbarouk Suleiman Mbarouk, Mohamed Khamis Juma na Masoud Amour Kombo, na waliotwaa fedha ni Omar Dola Abeid, Ali Juma Ali, Abdulsamad Alawi Abdallah na Mohamed Abdulrahman Mohamed.
Kwa upande wa wanawake, walioing'arisha timu ya Zanzibar ni Grace Alphonce (dhahabu1), pamoja na Lailati Khatib aliyetwaa medali ya fedha.
Mara baada ya kuwasili katika bandari ya Zanzibar, msafara wa timu hiyo ukaenda hoteli ya Bwawani kwa hafla ya kubezwa, ambapo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bihindi Hamad Khamis, alisema ushindi huo ni ushahidi wa vipaji vya michezo vilivyosheheni nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Issa Mlingoti Ali, alisema kazi iliyofanywa na vijana hao ni kubwa na inaiweka Zanzibar katika chati ya kimataifa, na kuahidi kuwa wizara itaandaa tafrija maalumu kuwapongeza pamoja na wanamichezo wengine walioiletea sifa Zanzibar.
Msafara wa timu hiyo ulijumuisha watu 25, wachezaji 20 na viongozi watano, ambapo ulipokelewa na watendaji wa wizara akiwemo pia Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis Salum 'Sherry'.
No comments:
Post a Comment