Habari za Punde

CHINA YATOA VIFAA VYA UPASUAJI MNAZIMMOJA HOSPITAL

Na Mwanajuma Abdi

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu China imesema imeweka kipaumbele kuimarisha sekta ya afya ili kuwapatia huduma bora wananchi katika kupambana na adui maradhi nchini. 


Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Chen Qiman alisema hayo, alipokabidhi msaada wa vifaa vya upasuaji vikiwemo vya macho na dawa mbali mbali kwa hospitali ya Mnazimmoja, ambapo Waziri wa Afya Juma Duni Haji alivipokea katika ukumbi wa Wizara hiyo mjini hapa.

Alisema huduma za afya zitaimarishwa ili ziweze kukidhi haja za kuwahudumia wananchi, sambamba na kuahidi kuifanyia matengenezo makubwa ICU (chumba cha wagonjwa mahatuti), ambapo watalaamu wa China watafika kwa ajili ya kuifanyia uhakiki pamoja na kuendeleza kuimarisha hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo kisiwani Pemba katika utoaji wa huduma kwa watu wa huko.

Alieleza China ina uhusiano wa muda mrefu na serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, katika kuwajengea uwezo watendaji na kusaidia misaada mbali mbali ya kimaendeleo ili kupambana na umasikini na kukuza uchumi.

Nae Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema huduma za afya zimeimarika mjini na vijijini kwa asilimia 95, ambapo watu hawatembei masafa marefu kwa kila kilomita tano vinapatikana vituo vya afya.

Alishukuru serikali ya China kwa msaada wa vifaa na madawa hayo ambayo yatasaidia kuimarisha huduma za matibabu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Aidha alisema Zanzibar na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ina uhusiano wa muda mrefu, ambao umekuwa chachu ya mafanikio makubwa katika sekta hiyo kuanzia wataalamu na upatikanaji wa vifaa na huduma mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.