WITO umetolewa kwa wafanyabiashara nchini kujenga na kutekeleza imani yao na kuwa na ihsani kwa kufanya biashara zao kwa kutowadhulumu wanunuzi kwa bei, vipimo au ubovu wa bidhaa wanazoziuza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dk. Ali Mohamed Shein, ameyasema hayo wakati akitoa risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu.
Katika risala hiyo Dk. Shein, alisema kuwa Serikali kwa kupitia vyombo na taasisi zake imeandaa mazingira mazuri ya kufanyia biashara za vyakula katika mwezi wa Ramadhani na kusisitiza haja ya kufanyiana wema na ihsani katika kipindi hicho chote.
Alisisitiza kuwa wauzaji sokoni na mitaani wanatakiwa watoe mashirikiano katika jambo hili, na kuzitaka Manispaa na Halmashauri kuzidisha bidii katika usafi wa miji.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa hali ya chakula inaendelea kuongezeka zaidi kutokana na wafanyabiashara kuongeza na kuagiza bidhaa zaidi ambapo katika hali ya kawaida bei ya bidhaa hizo hazitarajiwi kupanda ila kushuka kila mazao yanavyozidi kuingia sokoni.
Alieleza kuwa kutokana na kuimarika kwa biashara ya nje, hasa kutoka Dubai, bidhaa nyingi zinapatikana maduni hivi sasa kwa ajili ya Ramadhani na hata Sikukuu ya Idd El Fitri.
Dk. Shein alisema kuwa nguzo ya Saumu ina nguvu kubwa za kumuongoza mtu awe na tabia njema, uvumilivu na subira ambapo pia, alisisitiza haja ya utulivu, upendo, uvumilivu, umoja na kuwa na subira hata kwa wasio waislamu.
“Haya ni mambo ambayo tunapaswa kuyatafuta kwa nguvu na imani zetu ili tufanikishe Saum yetu.....misingi mikubwa ya mambo hayo ni imani na ihsani, tukiwa na ihsani tutakuwa Waumini na ndivyo tulivyoamrishwa na MwenyeziMungu katika Suratul Baqara, aya ya 183.
Aidha, mbali ya malipo ya saumu kutoka kwa MwenyeziMungu lakini yapo malipo yanayoonekana kila Ramadhani katika jamii ambapolisisitiza haja ya kuimarisha utulivu, upendo, uvumilivu, umoja na kuwa na subira hata kwa wasiokuwa waislamu.
Aidha, alisisitiza wajibu kwa waumini kuhudhuria na kuhimizana kwenda katika darsa na pia, kuwachukua vijana na watoto ili wapate misingi mizuri ya maisha sanjari na kuzidisha kusoma Qur-an tukufu katika mwezi wa Ramadhani.
Kwa upande wa huduma muhimu ya maji Dk. Shein alieleza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha kwamba kwa kipindi chote cha mwezi wa Ramadhani maji yanapatikana ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Nimeiagiza Mamlaka ya Maji na Wizara inayoshughulikia maji isimamie kwa karibu zaidi maeneo ya uzalishaji wa maji, upatikanaji na usambazaji, ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika.
Aidha, alieleza kuwa pindi tatizo la maji litakuwa kubwa Mamlaka ya maji kwa kushirikiana na wananchi isambaze maji kwa njia ya kutumia magari ili kuwawezesha wananchi kugfunga Ramadhani bila ya kupata usumbufu.
Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa viongozi na wananchi, hasa Masheha kuwa karibu zaidi na Mamlaka ya Maji katika kipindi cha Ramadhanikwa kutoa taarifa ya hali halisi ya maji katika maeneo yao kwa nia ya kufikia lengo la kuwahudumia wananchi wote.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza wananchi kuheshimu sana maadili ya Ramadhani, zaidi kwa wafanyabiashara wa vyakula, hoteli na mikahawa, aliwasihi kutambua wajiu wao katika Mwezi Mtukuu wa Ramadhani.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza kuwa ni lazima heshima ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iwepo kwa watu wote, bila ya hayo kunaweza kutokea kutofahamiana katika jamii na kuleta sura mbaya na kuvunja amani.
“Maadili ya asili ya mwezi huu Mtukufu yanajulikana vyema na ni vizuri tukayaenzi, tukatazane kwa upole na laima yawepo mafahamianolakni kwa uthabiti na dhamira njema”, alisema Alhaj Dk. Shein.
Dk. Shein pia, alitoa wito kwa wananchi kuweka mbele ihsani kwa kuwafikiria masikinji na wanahitaji wengine katika Mwezi wa Ramadhani ambapo aliyenacho hata kama ni kidogo basi amfikirie yule asiyekuwa na chochote.
Aidha, alisisitiza haja ya kujenga subira, uvumilivu, mapenzi na moyo wa kuhurumiana na kutekeleza ibada zote za Ramadhani kwa bidii na dhati ili kupatikane malipo kutoka kwa MwenyeziMungu.
No comments:
Post a Comment