Habari za Punde

KINIJU, KAJENGWA NAKO WAPINDUANA

Wadaiwa kuchoka na viongozi wazembe

Na Ameir Khalid

IKIONESHA kuchoshwa na viongozi wasiowajibika ipasavyo, hatimae timu ya Kiniju ya Makunduchi imeamua kufanya mabadiliko na kuteua viongozi wapya kuiongoza kwa nia ya kuiletea maendeleo.


Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya timu yenye maskani yake Kajengwa, zimesema kuwa hatua hiyo imeshinikizwa zaidi na matokeo mabaya katika ligi yaliyoifanya iporomoke kutika daraja la pili hadi la tatu.

Katibu Mkuu wa timu hiyo Seif Mrope, alifahamisha kuwa, maamuzi hayo magumu yalifikiwa katika kikao cha hivi karibuni, kwa lengo la kuwang'oa viongozi wazembe ambao wamesababisha timu hiyo kupoteza dira kwa miaka mingi.

Mbali na hatua hiyo ya kuwafyeka viongozi hao, Mrope pia alisema huo ni mwanzo tu kwani panga hilo litahusisha pia wachezaji kwa kuhakikisha Kiniju inafanya usajili makini msimu huu kwa kusaka wachezaji watakaoweza kuiletea mafanikio na kuwaweka kando wale wanaoonekana kuchoka.

Aliwataja viongozi waliochaguliwa kushika hatamu za kuiendesha timu hiyo, kuwa ni Abdalah Pondolo (Mwenyekiti), Haji Mwinyi Ussi (Ms. Mwenyekiti), huku nafasi ya Katibu Mkuu ikishikiliwa naye Seif Mrope akisaidiwa na Ali Issa Dalali.

Aidha katika kasha la hazina, amechaguliwa mwanamama Fatma Iddi kulishikilia ambapo msaidizi wake anakuwa Abdulla Dalo, huku Shukurani Islam akipewa dhamana ya umeneja na msaidizi wake ni Abdukadir Issa na Mohammed Tangisho (Katibu Mwenezi) akisaidiwa na Kheir Buna.

Pandu Hassan na Suleiman Kitundua wanakuwa washauri, mtunza vifaa ni Vuai Kindingu, walezi ni Idrisa Makame, Mohammed Haji na Vuai Kibuyu, huku benchi la ufundi likiongozwa na makocha watatu ambao ni Mtumwa Ameir, Mzee Obua na Issa Shagaa, na Ali Vuai amevishwa bendeji ya unahodha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.