Habari za Punde

RAMBIRAMBI ZAENDELEA KUTOLEWA

Na Mwandishi wetu

TAASISI mbali mbali nchini zimeendelea kutoa mkono wa pole kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander na kuua zaidi ya watu 150 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Ajali hiyo ilitokea katika mkondo wa bahari ya Nungwi majira ya saa 8 kuamkia Jumamosi iliyopita, ambapo ilikuwa ikitokea bandari ya Zanzibar na kuelekea Wete kisiwani Pemba.


BAKWATA

Kwa upande wake Baraza kuu la waislamu Tanzania (BAKWATA), limesema kuwa limepokea kwa mshituko taarifa kuzama kwa meli hiyo na kwaombea kwa Mwenyezi Mungu walazwe mahali pema peponi wale waliofariki na majeruhi kupona haraka.
Katika barua ya salamu hizo iliyosainiwa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shabani Simba alisema, “kwa niaba ya Baraza na waislam wote kwa ujumla namuomba Allah (S.w) awape moyo wa subra na uvumilivu wafiwa na wewe Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika kipindi hiki kigumu”.

JUWASEJMUTAZA

Jumuia hiyo ya wastaafu serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisema kuwa inatoa mkono wa pole kwa jamaa wote kwa ndugu na jamaa ambao wamepoteza maisha yao pamoja na kuwaombea majeruhi.
Katibu wa JUWASEJMUTAZA, Rashid Ali Juma, alisema jumuia ya wastaafu kama wazee inawaomba wale wote waliopata msiba huo kuwa na subira kwai tukio la kuzama kwa meli hiyo ni pigo kubwa kwa taifa.
“Tokeo hili ni pigo kubwa sana kwa taifa letu la Tanzania na pia ni msiba mkubwa sana kwetu”, alisema Juma.

ZSC

Bodi ya wasafirishaji wa mizigo (ZSC), imetoa mkono wa rambi rambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti 
wa Baraza la Mapinduzi kwa msiba mkubwa uliolikumbwa taifa.
“ Hivyo unaziomba familia, ndugu, jamaa na marafiki na Wazanzibari kwa ujumla kuwa na subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo”, ilisema taarifa hiyo.

UMAWA

Umoja wa Maaskari wastaafu (UMAWA), umetoa mkono wa rambi rambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein na wafiwa wote walipatwa na msiba wa kuzama meli ya Mv Spice Islander.
“Sisi wana UMAWA tumepokea kwa mshituko mkubwa tukio hili kwani hili ni tukio kubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba ambapo halijawahi kutokea”, ilieleza taarifa hiyo.

AFP

Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), katika salamu zake za rambi rambi kimetoa mkono wa pole Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa msiba uliolikumba taifa.
Mkurugenzi Mipango, Uendeshaji na Sera, Rashid Yussuf Mchenga alisema AFP inaungana na wananchi wote na familia za marehemu katika msiba uliolikumba taifa kufuatia kuzama kwa meli hiyo.

WAWAKILISHI

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, wametoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia kuzama kwa meli ya Mv Spice Islander.

Wajumbe hao walieleza hayo jana chini ya Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho, kufuatia kukutana katika kikao maalum cha dharura, ambapo mbali ya kumpa pole Dk. Shein pia walitoa salamu za rambirambi kwa wafiwa na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Wajumbe wa Baraza wanatoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wafiwa wote na wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambao kwa namna moja au nyengine wameathiriwa na msiba huo”, alisema.

Aidha, Spika Kificho aliwaomba wananchi wote kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maombelezo na kwa pamoja tumuombe Mwenyezi Mungu atusaidie.

Aidha wajumbe hao wametoa wito kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi zake, kuchukua hatua zote muafaka zinazohitajika katika wakati huu mgumu.

UN

Katika hatua nyengine naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemtumia salamu za rambirambi Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufuatia ajali mbaya ya kuzama kwa kivuko cha MV Spice Islander.

Katika salamu zake, Katibu Mkuu alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuzama kwa kivuko hicho katika pwani ya Zanzibar na kwamba Umoja wa Mataifa uko pamoja wananchi wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu na nakala yake kupatika Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Salamu za pole za Katibu Mkuu, pia anazituma kwa Serikali na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar na familia za waathirika wa ajali hiyo.

Katibu Mkuu Ban Ki Moon, pia aliwatakia kila la kheri na nafuu ya haraka majeruhi na wote walionusurika wa ajali hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.