Habari za Punde

WAJUMBE BARAZA LA WAWAKILISHI KUWATEMBELEA WAZEE ARUSHA

Wajumbe wapato 100 wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakiwemo mawaziri kumi na mbili na wakiongozwa na Spika wao Mhe. Pandu Ameir Kificho, wanawasili Arusha siku ya Alhamisi wiki hii kwa ziara ya siku nne wakiwa wamealikwa na Arusha Wazee Sports Club.


Mwenyekiti wa Wazee Club Danford Mpumilwa alisema jana kuwa ujumbe huo mzito unatembelea Arusha kwa ziara ya kimichezo pamoja na kutembelea taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zilizopo Arusha. Vilevile ujumbe huo utatumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya kitalii vilivyope hapo Arusha.

Mpumilwa alisema kuwa mkakati mzima ni kuimarisha uhusiano wa kindugu wa Muungano wa Tanzania pamoja na kuendeleza mahusiano ya kimataifa ambapo Arusha ni kitovu cha shughuli nyingi za kimataifa.

Alieleza kuwa ujumbe huo utakapokuwa Arusha, pamoja na sehemu nyingine, utatembelea Chuo kipya cha Kimataifa cha Mandela kinachoanza kuchukua wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika mwaka huu pamoja na kiwanda kipya cha Hughes hapo Usa River.

Vilevile ujumbe huo utatembelea mbuga ya wanyama ya Tarangire kabla ya kucheza mechi ya mpira na michezo mingine na wenyeji wao siku ya Jumapili hapo kwenye viwanja vya General Tyre.

Mpumilwa alisema kuwa Klabu ya Wazee ambayo inajumuisha wanachama wapatao 150 wanaoishi na kufanya kazi na biashara Arusha na ambao wanatoka mataifa zaidi ya 20 ni mfano bora wa kuendeleza mahusiano mazuri kitaifa na kimataifa.

Kila mwaka wajumbe wa Baraza la wawakilishi hutembelea Arusha mara tu baada ya Bunge la bajeti na Wazee wa Arusha hufika Zanziba wakati wa sherehe za Pasaka.

Klabu ya Wazee sasa hivi ina mahusiano na Bunge la Jamhuri ya Kenya na iko mbioni kuanzisha mahusiano ya karibu na Bunge la Uganda. Hii ni juu ya kuwa na mahusiano ya kimichezo na vilabu vya kimichezo vilivyopo Dar es Salaam, Nairobi, Moshi, Tanga na Arusha yenyewe.

1 comment:

  1. Jambo la maana sana,nasikia Arusha kumekucha kweli kweli kimaendeleo huenda watu wetu wakajifunza na kurudi na mambo mapya nyumbani...wasisahau makoti tu na mjaket!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.