Habari za Punde

WILAYA TANO ZA UNGUJA NA PEMBA ZIMEATHIRIKA NA UGONJWA WA SURUA

Na Hamad Hija-Maelezo Zanzibar

IMEELEZWA kuwa jumla ya Wilaya tano za Unguja na Pemba zimeathirika na ugonjwa wa surua ambao umetokea hivi karibuni hapa Zanzibar ambapo watoto 262 wameripotiwa kuathika na ugonjwa huo.


Waziri wa Afya wa Zanzibar Juma Duni Haji aliyaeleza hayo wakati akitowa taarifa ya Wizara yake kwa waandishi wa habari kuhusiana na mripuko wa ugonjwa huo ambayo umeikumba Zanzibar.

Amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa Septemba jumla ya watoto 262 kutoka wilaya mbali mbali za unguja na Pemba walikuwa wameathirika na maradhi hayo ambapo kati ya wagonjwa hao 222 wamepatiwa matibabu katika hospital za hapa zanzibar.

Waziri Juma Duni amesema kuwa wamebaini kwamba miongoni mwa waathirika wakubwa wa ugonjwa huo ni wale ambao hawakukamilisha chanjo ya ugonjwa huo wa surua.

Aidha amesema Wizara yake imepanga kuuanzia Jumatatu inayofuata kufanya kampeni kubwa ya kutowa chanjo juu ya watoto wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi miaka mitano.

Waziri huyo wa afya amezitaja Wilaya ambazo zimeathirika na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na Wilaya ya Micheweni,Wete, Mkoani na Chake Chake kwa upande wa Pemba na kwa upande wa Unguja ni Wilaya ya Mjini na Magharibi ambapo hadi leo hakuna mtoto alyefariki kuhusiana na suala hili

Kutokana hali hii ya kukabiliwa na ugonjwa huu wa surua Wizara ya Afya inaiarifu jami kuwa inakabiliwa na tatizo kubwa la maradhi haya hivyo jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na maradhi haya hatari ambapo suala kubwa na muhimu ni kuwapeleka watoto kwenda kupata chanjo vituoni.

Aidha Waziri Juma alisema kuwa katika kukabiliana na suala hili jamii ihakikishe kuwa watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi miaka mitano wanachanjwa haraka iwezekanavyo

Alisema mbali na jamii na familia kuwachanja watoto wao pia kuna haja kubwa kwa viongozi wa dini na wanasisa kusaidia kushajiisha na kutowa elimu juu ya ugonjwa huu wa surua uliopo hapa nchini.

Akizungumzia juhudi ambazo zinachukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa huu alisema kuwa wizara imeunda kikosi kazi ambacho kitakuwa mstari wa mbele katika kushughulikia suala hili

Aidha wanawachanja watoto kuanzia miezi sita hadi miaka mitano na kushiririkiana na mashirika ya umoja wa kimataifa kama vile WHO na UNICEF katika kupanga mipango sahihi ya kukabiliana na miripuko hiyo ya surua.

Wakati huo huo Waziri amewataka waandishi wa habari kuchukuwa juhudi za makusudi kwa kutowa taaluma juu ya ugonjwa huo ili ziweze kuwafikiya walengwa na katika kuhakikisha kuwa wanautokomeza Ugonjwa wa Surua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.