Habari za Punde

DK SHEIN AZINDUA TAWI LA PBZ CHAKECHAKE PEMBA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akizungumza na wananchi wa Chake Chake kisiwani Pemba wakati wa uzinduzi wa tawi la Benki ya PBZ

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein,akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Tawi la Benki ya PBZ huko Chake Chake Pemba,(kushoto) Mkurugenzi wa PBZ Juma Amour na (kulia) Kaimu Waziri wa Fedha Mhe,Mwinyihaji Makame

Picha na Ramadhan Othman, Pemba



HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA
MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DKT. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA HAFLA YA UZINDUZI WA JENGO JIPYA LA
BENKI YA WATU WA ZANZIBAR TAWI LA CHAKECHAKE
TAREHE 31 OKTOBA, 2011


Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na pia Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo,
Mhe. Juma Kassim Tindwa, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,
Mhe. Abdulrahman Mwinyijumbe, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Viongozi mbalimbali,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Assalam Aleykum

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu (S.W) kwa kutujaalia kuwepo hapa tukiwa na afya njema na nchi yetu ikiwa katika hali ya amani na utulivu.



Vilevile, natoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kunipa heshima ya kulizindua jengo lenu jipya hapa Chakechake. Nakiri kuwa jengo tulilolizindua muda mfupi uliopita ni zuri, lenye hadhi na la kisasa. Kwa hakika linameremeta na limeongeza haiba ya mji wa Chake Chake. Hongereni sana.

Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa madhumuni makubwa ya kuanzishwa kwa Benki hii ni kuleta maendeleo kwa jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa jumla. Nimefarajika sana kuona kuwa Benki ya Watu wa Zanzibar ya sasa siyo Benki ya Watu wa Zanzibar ya miaka kumi iliyopita. Benki ya Watu wa Zanzibar ni moja ya Taasisi zilizochini ya umiliki wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na maendeleo yake yanaonekana kuwa mazuri siku hadi siku. Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hii ni kielelezo kinachodhihirisha jinsi Benki hii inavyopiga hatua mbalimbali za maendeleo.

Nimefurahi kusikia kuwa amana za wateja zimekuwa zikiongezeka kila mwaka ambazo hadi kufikia Septemba, 2011 zimefikia shilingi bilioni 139.3. Kuongozeka kwa amana hizo kunaashiria jinsi Wazanzibari na Watanzania kwa jumla wanavyopenda kuitumia Benki hii na wanaridhika na huduma zake.

Nimefarajika kwamba Benki hii imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali ya biashara na pia mikopo kwa wafanyakazi wa Serikali ambapo hadi tarehe 30 Septemba, 2011 mikopo ya shilingi bilioni 52.2 tayari imeshatolewa. Mikopo hiyo ni muhimu kwetu katika kuimarisha maendeleo na kuinua maisha ya wananchi na kupunguza umaskini. Wafanyakazi wengi wanaendelea kufaidika na mikopo hiyo kwa kuimarisha ujenzi wa makaazi yao, kugharamia matibabu, masomo na kadhalika. Hivyo utoaji wa huduma za mikopo kwa maendeleo ya wananchi unakwenda sambamba na madhumuni ya kuanzishwa kwa Benki hii na pia unatekeleza lengo la Serikali la kuwawezesha wananchi.

Ndugu Wananchi,
Ni jambo la fahari na kutia moyo kwamba Benki ya Watu wa Zanzibar imeweza kuimarisha huduma zake kutoka mifumo ya kizamani na kuweka mifumo ya kisasa na kuweza kukabiliana na ushindani wa mabenki yaliopo hapa Tanzania. Miongoni mwa mifumo hiyo ni kuweka mfumo wa usafirishaji wa fedha kwa njia ya haraka (Swift) na kuweka mtandao wa kutoa fedha (ATM) kwa saa ishirini na nne (24), ambayo ni muhimu katika maisha ya sasa, hasa kwa shughuli za kibiashara.

Aidha, nimefarijika sana kuona Benki inaongeza wigo wa shughuli zake sehemu mbalimbali za Zanzibar na Tanzania Bara. Ndani ya mwaka huu (2011), Benki tayari imeshafungua vituo vyake viwili katika Wilaya za Wete na Mkoani na pia imeongeza matawi yake kutoka matatu (3) hadi matano (5) katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na matawi mawili (2) katika Mkoa wa Dar es Salaam ambayo yapo katika maeneo ya Kariakoo na Lumumba. Utanunzi huo wa matawi unadhihirisha azma ya Benki hii kuwa karibu na jamii ambalo ni jambo zuri linalopaswa kuendelezwa.

Ndugu Wananchi,
Matokeo yote hayo ya ukusanyaji wa amana za wateja, kutoa mikopo kwa uadilifu, kuimarisha huduma za Benki kwa kutumia mifumo ya kisasa pamoja na kutanua wigo wa shughuli zake sehemu mbalimbali nchini Tanzania kumesababisha Benki hii kuwa na nafasi nzuri kiutendaji. Hali hiyo inathibitishwa na kuimarika mtaji wa Benki siku hadi siku. Benki ilikuwa haina mtaji katika miaka ya mwanzoni mwa 2000 na sasa mtaji wake umeshafikia zaidi ya shilingi bilioni 15.

Kwa hatua zote hizo za maendeleo naipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Uongozi na wafanyakazi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kusimamia na kutekeleza vizuri shughuli zao. Kwa upande mwengine nawapongeza wateja na wananchi wote kwa jumla kwa kuendelea kuitumia Benki yao.

Kuongezeka kwa mabenki nchini na Taasisi nyengine zinazohusika na masuala ya kibenki kama vile vituo vya kubadilishia fedha (Bureau de Change), huduma za kutuma pesa kwa simu kama vile M-Pesa ni kielelezo cha kuimarika shughuli za kiuchumi. Hivi sasa Zanzibar ina Mabenki yapatayo kumi na vituo vya kubadilishia fedha kadhaa. Hata hivyo, kwenu nyinyi ni changamoto ya ushindani uliopo. Kwa hivyo, mna wajibu wa kutumia taaluma zenu kuukabili ushindani kwa kuimarisha huduma zenu. Natoa rai Benki iangalie uwezekano wa kujenga nyumba za bei nafuu na kuwakopesha wananchi. Hata hivyo, ni vyema mkajipanga kwanza. Wahenga walisema, “kupanga ni kuchagua”.


Ndugu Wananchi,
Jengo hili limejengwa kukidhi ushindani wa mabenki uliopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla. Tumefahamishwa kuwa sehemu ya juu itakuwa ikitoa huduma za Benki ya Kiislam na sehemu ya chini itatoa huduma za Benki zinazotolewa kikawaida. Tunaupongeza Uongozi wa Benki kwa kuanzisha huduma za Benki ya Kiislam ambazo sasa zinakubalika na kuenea katika nchi nyingi, hata za Ulaya.

Huduma hizo zinaendelea kusambaa katika nchi kadhaa ulimwenguni kama vile Malaysia, Singapore, Kenya na kadhalika. Nimefurahi kuona Benki ya Watu wa Zanzibar imefungua ukurasa mpya katika kutoa huduma hizo za Benki ya Kiislamu na nina imani kuwa huduma hizo zitawafaa wananchi wa Tanzania na kwamba zitakuwa ni chachu ya kusaidia maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Elimu kwa wananchi juu huduma hizi zinahitajika sana kwa sababu ni mpya kwa jamii ya Wazanzibari na Tanzania kwa jumla. Huduma hizi zimeingia nchini hivi karibuni. Ninaamini kadiri elimu itakavyotolewa kwa wananchi ndivyo huduma hizo zitakavyotumiwa zaidi kwani “usilolijua ni usiku wa kiza”. Nimefarijika kusikia kuwa wateja wa huduma za Benki ya Kiislamu inafikia 5,700. Huu ni mwanzo mzuri kwani “nyota njema huonekana alfajiri”.

Ninaupongeza tena Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kutokana na mipango yao ya miaka inayofuata ya kujenga Makao Makuu Mapya ya Benki, kueneza vituo na matawi katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na Tanzania Bara. Pamoja na pongezi hizo napenda kutoa nasaha zangu zifuatazo:-
Ujenzi wa Makao Makuu Mapya usicheleweshwe. Tukijaaliwa katika mwaka 2012 Serikali inataka kuona Benki ya Watu wa Zanzibar inaanza ujenzi wa jengo la Makao Makuu. Tunataka kuona kuwa Benki hii ina jengo la Makao Makuu jipya na la kisasa linaloendana na hadhi ya benki yenyewe na matawi yanayofunguliwa. Kwani siku zote “nguvu ya mti shinani”.

Kuhusu utanuzi wa matawi ya Benki, endeleeni kujitanua kwa mujibu wa mipango yenu. Hata hivyo, napenda kutoa ushauri juu ya ufunguzi wa matawi mengine. Itakumbukwa kuwa katika miaka ya 1990 Benki hii ilifungua matawi mengi Unguja na Pemba. Baada ya kuonekana kuwa matawi hayo yanaendeshwa kwa hasara, ilibidi yafungwe. Hivyo ushauri wangu kwenu ni kuhakikisha kuwa matawi hayo yanafunguliwa katika maeneo yenye harakati nzuri za kiuchumi ili kuepuka kurudia makosa yaliyofanyika siku za nyuma.

Nasisitiza sana suala la kulitunza jengo hili. Hili ni jukumu la wafanyakazi na pia wananchi ambao ndiyo wateja wenyewe. Wahenga walisema “kitunze kidumu”. Nasi tunawajibu wa kulitunza jengo hili; ili lidumu na hadhi yake kwa muda mrefu zaidi.

Ndugu Wananchi,
Mimi binafsi naamini kuwa juhudi zote hizi ni kujaribu kuifanya benki hii kuwa Benki ya Watu wa Zanzibar kwelikweli. Imani hio niliyonayo inathibitishwa na juhudi uongozi wa benki za kufungua matawi mengi zaidi kila walipo Wazanzibari kwani ndiyo wenyewe. Pili, huduma za benki hii zinazingatia pia utamaduni wa Wenyewe Wazanzibari. Ndio sababu bila ya kuchelewa Benki hii ikaona haja ya kuanzisha huduma za Kiislam.

Jambo kubwa zaidi ya yote ni mlahaka na ukarimu wa wafanyakazi wa Benki hii. Wafanyakazi hao ni mahodari na wanajua hasa kumpembejea mteja ndio sababu wateja wake wanaongezeka kila siku. Nawanasihi sana wananchi wazitumie huduma hizi za Benki ya Watu wa Zanzibar.

Tawi hili limefunguliwa wakati msimu wa uchumaji karafuu unaendelea. Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) limeshatumia zaidi ya shilingi bilioni 25.7 kununulia karafuu hapa Pemba kutoka kwa wakulima. Nyingi ya fedha hizi ziko mikononi jambo ambalo ni hatari sana. Ni vyema wananchi tukaitumia fursa hii kuzilinda fedha zetu na kujiwekea akiba kwa siku zijazo. Msanii mmoja alisema “akiba si ubakhili, hufaa siku ya pili”. Lazima tujenge utamaduni wa kujiwekea akiba.

Kwa hakika siyo jambo la busara hata kidogo kukaa na fedha nyingi nyumbani au kusafiri nazo kwa kuchelea majanga mbalimbali. Kuweka fedha benki ni kuzifanya ziwe salama na kwa vile benki yetu ina matawi sehemu mbalimbali mtu ana fursa ya kuzitoa kwenye matawi yao popote na kwa sasa wakati wowote kwa kutumia huduma ya ATM.

Ndugu Wananchi,
Mwisho kabisa napenda kuwasisitiza tena wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa kutumia Benki kwa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhifadhi fedha na kutuma fedha sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa usalama wao na mali zao.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa jengo jipya la Benki ya Watu wa Zanzibar Tawi la Chakechake limezinduliwa rasmi.

Ahsanteni Sana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.