Habari za Punde

JIHAD AWAAMBIA WANANCHI WA PEMBA WATAONA TVZ MWISHO WA MWEZI

Ataka ZBC ilipe malimbikizo posho wafanyakazi

Na Abdi Shamnah

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar (WHUUM), Abdillah Jihad Hassan, amewataka wananchi kisiwani Pemba, kuwa na subira huku akisema kuna matumaini makubwa ya matangazo ya Televisheni kurejea upya kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Ametoa kauli hiyo jana Karume House, alipokuwa na mazungumzo kati ya watendaji wa Wizara yake na wale wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya kazi za ufungaji mitambo inavyoendelea kisiwani Pemba.


Alisema taarifa za maendeleo ya kazi za ufungaji wa mitambo zinatoa matumaini makubwa kwa kazi hiyo kukamilika siku chache zijazo na mitambo hiyo kufanyiwa marekebisho kabla ya mwezi huu kumalizika.

Akizungumzia juu ya utendaji wa kila siku wa shirika, Waziri Jihad aliwataka watendaji hao kuzingatia na kusimamia maadili ya kazi za utangazaji kwa kuzipitia Programu zote (Editing) kabla ya kurushwa hewani.

Alisema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi ya kituo hicho kuhusishwa na uoneshaji wa vipindi visivyozingatia maadili ya Kizanzibari ikiwemo filamu, muziki na lugha za mitaani na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha za sahihi zinazokubalika na jamii.

Aidha alishauri kuwepo programu za mapema kwa vipindi vinavyotoa taaluma ili viweze kuwafaidisha walengwa, badala ya kupangiwa nyakati za usiku muda ambao alisema watu wengi wanakuwa tayari wameshapumzika.

Katika hatua nyingine Waziri Jihad aliujia juu uongozi wa Shirika ZBC na kuutaka kufanya juhudi za dharura kulipa posho za wafanyakazi wa shirika waliokwenda masomoni nchini Uholanzi 2005.

Alisema kuna taarifa kuwa wafanyakazi 20 wa kituo cha Televisheni Zanzibar waliokwenda masomoni Uholanzi 2005 walilipwa nusu ya posho walilostahiki, huku kila mmoja akidai Sh.500,000/- hadi leo.

Aidha aliitaka menejment ya Shirika hilo kufanya juhudi kuwalipa maposho yao wafanyakazi walioshiriki vikao vya Baraza la Wawakilishi vilivyopita, ili kuondoa manung’uniko.

Alisema kitendo cha kutowalipa kwa wakati wafanyakazi wanaoshiriki vikao hivyo, hakileti picha nzuri kwa Shirika hilo kwa kuzingatia kazi kubwa wanayoifanya.

Vile vile aliutaka uongozi huo kutoa taaluma kwa wafanyakazi wake ili wafahamu ni nanai hasa wwanaopaswa kulipwa posho hizo.

Nae Naibu Waziri WHUUM, Bihindi Hamad aliukumbusha uongozi huo umuhimu wa kuhakikisha wafanyakazi wanaoshiriki vikao katika Baraza la Wawakilishi wanakuwa nadhifu.

Alisema ni lazima ihakikishwe kuwa wafanyakazi hao wanapatiwa nguo rasmi (suti) ili kuendana na hadhi ya chombo hicho muhimu katika Taifa.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa ZBC, Hassan Mitawi akitoa ufafanuzi juu ya baadhi ya masuala, alisema shirika lake linaendelea na juhudi za kutafuta vyombo na taasisi wahisani (ikiwemo Deutse Welle) kusaidia mafunzo ya muda mfupi kwa watendaji wake juu ya matumizi ya mfumo wa digital.

Alisema kuna umuhimu wa kuendelea kuwaelimisha wataalamu wazoefu waliopo, ambao pamoja na kuwa na uelewa mkubwa katika matumizi ya mfumo wa Analogi, ni rahisi kwao kufundishika kuliko kutafuta watu wapya.

Alisema katika kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana wakati huu wa ushindani, Shirika linajipanga kuimarisha vipindi vya “Roving reporter” kwa lengo la kuwashirikisha moja kwa moja wananchi na kuwa sehemu ya vipindi hivyo.

Alisema ili kufikia dhana hiyo, Shirika linahitaji kuwa na watendaji wazuri na kusisitiza umuhimu wa kuajiri vijana wazuri, kuwa na mikataba madhubuti pamoja na kuwalipa vyema ili kulinda rasilimali watu isipotelee kwengineko.

Mitawi alieleza kuwa shirika limeweka mipango mizuri ya kuyakusanya magari yote (kutoka STZ na TVZ) ili yafanye kazi kwa pamoja, huku mipango ikiendelea kuimarisha kitengo cha usafiri.

Alisema Shirika linalenga kukabiliana na matumizi mabaya ya magari ili kuokoa fedha nyingi kutokana na matumizi binafsi, akisisitiza lengo la shirika kutafuta fedha na kuzitunza fedha hizo kwa kufanya matumizi mazuri.

Mapema, Fundi Mkuu wa kituo cha TVZ, Ali Muhsin alisema bado vituo vya Televisheni Zanzibar havijaanza rasmi matumizi ya mfumo wa Digital, ingawaje kwa kiasi kikubwa vifaa vilivyopo ni vya mfumo huo.

Aidha alisema suala la kukatikakatika kwa matangazo katika kituo cha Karume House, linatokana na uchakavu wa mashine katika studio iliyopo.

Akigusia tatizo la usafiri, Muhsin alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya magari kuambatana na kazi, huku kukiwa na tatizo la uchakavu wa magari.

Alisema hali ilivyo hivi sasa ni mbaya, hususan katika sehemu ya ufundi, kiasi ambacho baadhi ya wakati wafanyakazi (mafundi) hulazimika kulala katika kituo cha kurushia matangazo Dole, kutokana na ukosefu wa usafiri nyakati za usiku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.