Habari za Punde

MAVETERANI WA SOKA USWISI WAWASILI

Kukutana na Waziri Jihad VIP Bwawani

Na Salum Vuai, Maelezo

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA), kimetangaza ratiba ya ziara ya timu ya wanasoka wa zamani kutoka Uswisi, inayotarajiwa kuwasili kisiwani hapa leo mchana.

Msaidizi Katibu wa ZFA Masoud Attai amewaambia waandishi wa habari kuwa, msafara wa timu hiyo inayokuja kwa madhumuni ya kisoka, biashara na utalii, utafika bandarini saa 6:00 mchana kwa boti ya Kilimanjaro ukitokea Dar es Salaam ambako ilitarajiwa kuwasili jana usiku.


Attai alisema, watakapokuwa hapa, wachezaji wa timu hiyo, mbali na kucheza mechi za maonesho na baadhi ya timu, pia watapata fursa ya kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Abdilahi Jihad Hassan.

Alisema mkutano huo utakaojikita katika kubadilishana mawazo na kujadili njia bora za kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo, utafanyika katika ukumbi wa VIP hoteli ya Bwawani mnamo saa 10:00 jioni kesho.

Ziara ya wanandinga hao wa zamani, itahusisha kufanya mazoezi na timu ya akademi ya Fairmont, kucheza mechi na timu ya Wazee Sports ya Zanzibar pamoja na timu teule ya taifa ‘The Zanzibar Heroes’, na mabingwa wa Central taifa, Oranje Football Academy kwa siku tafauti.

Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria ikiwa pamoja na kufanya ziara kisiwani Pemba, timu hiyo itaagwa kwa tafrija maalumu Oktoba 27, itakayofanyika katika hoteli ya Tembo wakati wa usiku, ambapo kutakuweko maonesho kadhaa ya utamaduni huku Waziri Jihad akiwa mgeni rasmi.

Msafara huo unatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 28, kurudi Uswisi.

Attai ameeleza kuwa, kuja kwa timu hiyo ni fursa nzuri kwa wanasoka chipukizi wa Zanzibar na hata wakubwa na wastaafu, kufahamu mbinu mbalimbali za kisoka hasa kutokana na tafauti kati ya Zanzibar na Ulaya katika mchezo huo.

Aidha ujio wa timu hiyo unatarajiwa kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiutalii kati ya Zanzibar na Uswisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.