Na Mwantanga Ame
BALOZI Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar, Chen Qiman, amesema ili wazanzibari wawe pamoja na serikali yao watahitaji kupata mchango mkubwa kutoka kwa watendaji wa Serikali ya Zanzibar wanaoshiriki katika mafunzo mbali mbali nchini China, kwani ndio njia pekee ya msingi wa mabadiliko ya mendeleo ya Zanzibar.
Balozi Qiman aliyasema hayo jana uwanja wa ndege wa Zanzibar, baada ya kuupokea ujumbe wa Watendaji 24 wa Serikali ya Zanzibar waliokuwa wakishiriki katika mafunzo ya Usimamizi wa Raslimali Watu, yaliyokuwa yakifanyika nchini China kwa udhamini wa serikali ya China.
Balozi Qiman, alisema anaamini kuwa mafunzo waliyopewa watendaji hao yatakuwa ni moja ya dira ya msingi itayoweza kuleta mabadiliko ya utendaji kwa kuifanya jamii kuwa pamoja na serikali yao ikiwa ni hatua ya kuweza kufikia maendeleo zaidi.
Alisema kazi kubwa ambayo watahitajika kuifanya watendaji hao ni kuona wanaandaa ripoti itayoweza kuyaonesha maeneo muhimu ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ikiwa ni hatua itayoiwezesha serikali ya China kuyatambua na kufikiria kuyasaidia.
Alisema hatua hiyo pia itaweza kuisaidia nchi kuweza kutambua aina ya makundi ya watendaji wa serikali katika kuwapatia mafunzo zaidi ikiwa ni jambo la msingi katika kufanikisha mipango ya serikali.
Alisema anaamini kuwa sehemu kubwa ya macho ya wazanzibari hivi sasa yamekuwa yakiwaangalia watendaji wa serikali kuona vipi wataweza kuwapatia mabadiliko kupitia serikali yao.
Kutokana na hali hiyo, Balozi huyo, alilisitiza uwepo wa ripoti nzuri kwa watendaji waliomaliza mafunzo hayo ni jambo muhimu na ni la lazima kwani ndilo litaloweza kuifanya nchi hiyo kuandaa mipango bora ya kuisaidia Zanzibar.
Balozi huyo alisema serikali ya China imekuwa ikishirikiana na serikali ya Zanzibar kutokana na kuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kupenda kuiona Zanzibar kila siku inakuwa na mabadiliko ya maendeleo kwa vile uhusiano huo ni wa kihistoria.
Mapema Mkuu wa msafara huo, Kamishna Seif Shaaban, akitoa shukrani kwa Balozi huyo alisema mafunzo waliyopata katika kipindi cha siku 20 ni msaada mkubwa kwa serikali ya Zanzibar kwa vile utaweza kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha usimamizi wa raslimali watu.
Alisema ili kuweza kuleta mabadiliko ipo haja kwa serikali kuweza kuyatumia mafunzo hayo kwani yamewaonesha kuwepo kwa maeneo mengi ya maendeleo ambapo Zanzibar bado haijayafikia katika suala zima la kutumia raslimali watu.
Hata hivyo Kamishna Seif aliupongeza Ubalozi wa China uliopo Zanziabar na serikali ya China kuweza kuandaa mafunzo hayo kwa watendaji wa Zanzibar na kutaka kuendeleza ushirikiano huo kwa kutoa mafunzo zaidi.
Mafunzo ambayo watendaji hao wameyapata ni pamoja namna ya kuwatumia wataalamu wanaopewa mafunzo na serikali kwa kuwapelekea katika Miji ambayo haina maendeleo.
Eneo jengine ambalo wamepatiwa mafunzo hayo ni pamoja na namna ya kuishirikisha jamii kuwa karibu na serikali yao kwa kutumia raslimali watu, kuimarisha miundombinu, namna ya kuitumia idadi ya watu, muundo wa serikali za mitaa na kazi zake, upeo wa viongozi katika kuwatumikia jamii na serikali yao na kuendesha serikali kwa njia ya busara na kukuza uchumi.
Katika mafunzo hayo watendaji hao pia walipata bahati ya kutembelea maeneo ya vitega uchumi vya historia ya nchi hiyo ukiwemo wa eneo la Jumba la Mwenyekiti wa kwanza wa taifa hilo Mao Tse Tung ambalo lililokuwa likitumiwa na wafalme mbali mbali wan chi hiyo pamoja na kupanda mlima maarufu nchini humo ‘The Great Wall’.
Katika uwanja wa ndege watendaji hao kwa upande wa serikali ya Zanzibar walipokelewa na Kamishna wa Fedha za Nje katika Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Saada Mkuya
No comments:
Post a Comment