Habari za Punde

JIHAD AIAGA ZANZIBAR HEROES NA KUSEMA

Uwezo mnao msituangushe

Na Salum Vuai, Maelezo

WACHEZAJI wa timu ya soka ya taifa 'The Zanzibar Heroes', wametakiwa wasiwaangushe Wazanzibari katika mashindano ya Chalenji yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya kuiaga timu hiyo iliyofanyika jana kwenye ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mnazimmoja, Waziri wa wizara hiyo Abdilahi Jihad Hassan, alisema ni imani yake na wananchi wote kuwa kikosi hicho kimeiva na kina uwezo mkubwa wa kurudi
nyumbani na ubingwa.


Aidha alisema kutokana na maandalizi mazuri waliyopata kwa kupiga kambi ya wiki mbili nchini Misri, timu hiyo ni nzuri na inatisha mbele ya timu pinzani, na hivyo kuitaka ioneshe matunda ya kambi hiyo iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Jihad aliwataka wanandinga hao wasiziogope timu watakazopambana nazo kwani zote wamezizoea kwa kuwa wamekuwa wakikutana nazo kila wakati wa michuano hiyo unapofika.

"Hamna haja ya kuogopa, kwani hizo timu zinakuogopeni nyinyi, kwa ufupi mnatisha, nendeni mkiwa na lengo moja nalo ni kuleta kombe nyumbani", alishajiisha.

Aidha aliwahimiza kuzingatia sheria za mchezo na nidhamu, pamoja na kuwa makini na mbinu zinazoweza kutumiwa na wapinzani kuwatoa katika mchezo kisaikolojia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Future Century Hellen Masanja, alieleza kuwa kwa kushirikiana na wadau wengine wa michezo waliokubali kuchangia udhamini wa timu hiyo, wanajivunia mafanikio na kuimarika kwa kikosi hicho, na kwamba hana shaka kitafanya vizuri na kuiletea sifa nchi yao.

Alizishukuru kampuni na taasisi zote zilizojitokeza kuungana mkono na kampuni yake katika udhamini wa timu hiyo, sambamba na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kutoa ushirikiano mkubwa na kuongoza hafla ya chakula cha
usiku Machi 26, mwaka huu, ambayo ilifungua milango ya kuijengea mazingira mazuri timu hiyo.

Nahodha wa timu hiyo Aggrey Morris, aliahidi kuwa, wakiwa mashindanoni, watafanya kila wawezalo ili kulinda heshima ya Zanzibar kwa kushinda kila mchezo na hatimaye kurudi nchini na ubingwa.

Jumla ya wachezaji 20 wa timu hiyo waliondoka jana baada ya kukabidhiwa bendera, kwenda Dar es Salaam tayari kwa ngarambe hizo zinazodhaminiwa na kampuni ya bia 'Tusker Lager', wakiongozwa na
Mrajis wa Vyama vya Michezo Zanzibar Mustafa Omar, Mjumbe wa ZFA Pemba Hafidh Muhidin, pamoja na kocha Hemed Suleiman'Moroko' na Abdelfatah Abbas.

Timu hiyo iliyopangwa kundi B pamoja na Burundi, Uganda na Somalia, inatarajiwa kutupa karata yake ya kwanza kesho saa 10:00, kwa kuivaa Uganda kwenye uwanja wa taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.