MKURUGENZI Mkuu Wizara ya afya, Dk. Malik Abdalla Juma ameipongeza kampuni ya Tiens inayojihusisha na utengenezaji virutubisho vya afya mwilini.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar jana alipokuwa akifungua mkutano maalum wa utambulisho wa kazi za kampuni ya Tiens.
Alisema hatua ya Kampuni hiyo ya kutoa tiba mbadala kwa wananchi inasaidia kupata dawa muafaka kutokana na maradhi kadhaa yanayowasumbua.
Alifahamisha kwamba kampuni hiyo pia inasaidia Wizara ya afya upatikanaji wa matibabu ya uhakika kwa wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo aliwahimiza wananchi kuendelea kupima afya zao ili kuhakikisha wanabaini maradhi yanayowadhoofisha na kupatiwa tiba mapema badala ya kusubiri yawe yamewatopea ndipo watafute tiba.
Kwa kuzingatia umuhimu wa suala la tiba, aliwahimiza wananchi kutumia dawa hizo kwa vile tayari zimekubaliwa na serikali kuwa muafaka kwa maradhi mbali mbali.
Mkurugenzi huyo alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na afya bora ili waweze kumudu kufanya kazi mbali mbali za kujipatia rizki zao.
"Suala la afya ni muhimu hasa ikizingatiwa kuwa jamii inatawaliwa na maradhi mbali mbali yatokanayo na uhaba wa virutubisho vya mwili," alibainisha Dk. Malik.
Dk. Malik alisema jukumu la kulinda afya ni la kila mwananchi na sio serikali pake yake, hivyo ni vyema wananchi kuunga mkono juhudi za Kampuni hiyo na kutumia virutubisho mbadala ili kuepukana na maradhi mbali mbali.
Akizungumza katika mkutano huo, Meneja Masoko wa Kampuni hiyo Tanzania Zainab Mziray, amewataka wanachama na wasambazaji dawa wa kampuni hiyo, kujitahidi kutafuta masoko zaidi ya tiba za kampuni hiyo.
Kampuni ya Tiens inayojishughulisha na tiba mbadala za virutubisho kwa kugundua maradhi kupitia mashine maalum, inatoa huduma kwa takriban miaka miwili sasa na makao yake makuu yako nchini China ambapo tawi lake kuu liko Dar es salaam na hapa Zanzibar lipo Kiponda.
No comments:
Post a Comment