Na Salum Vuai, Maelezo
KATIKA hali ya kushangaza, Makamu Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Haji Ameir Haji, ameiponda barua ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ya kulibwaga ombi la Zanzibar kutaka uanachama, na kusema haikuwa rasmi.
Ameir alikuwa akizungumza katika kipindi cha televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar cha 'Sports Michezo', kinachorushwa kila Jumamosi saa 3:00 usiku, mwishoni mwa wiki.
Akitoa ufafanuzi juu ya suala aliloulizwa kuhusu mchakato wa Zanzibar kujiunga na FIFA baada ya shirikisho hilo kulitupilia mbali ombi lililowasilishwa na ujumbe wa nchi hiyo mwezi Septemba, 2010, Ameir
alidai kuwa, barua hiyo ya Juni 21, mwaka huu kutoka Zurich, si rasmi.
Katika hali iliyoonesha kutokufahamu alichokuwa akikisema, Makamu huyo wa Rais wa ZFA alidai kuwa, yeye ndiye aliyemuomba Rais wa FIFA Sepp Blatter aiandikie barua Zanzibar kuhusiana na ombi lake.
Hata pale alipoulizwa kama alimuagiza bosi huyo wa FIFA aandike barua hiyo kwamba ombi la Zanzibar limekataliwa, kiongozi huyo alishindwa kujibu vyema, na badala yake kumshambulia mmoja wa watu waliopiga simu kuuliza masuala ambaye ni mwandishi wa habari, kwamba amekuwa
akikiandika vibaya chama chake.
"Nasema barua iliyoletwa kutoka FIFA si rasmi, kimsingi mimi ndiye niliyemwambia Blatter atuandikie barua hiyo. Huyu (akitaja jina la mwandishi), ndiye anayeiandika ZFA vibaya", alieleza akionesha kuelemewa.
Kauli hiyo ya Ameir, imekuwa ya kushangaza kwani inafahamika wazi kuwa ZFA ilipelekewa barua ya Juni 21, 2011 kutoka FIFA, ikijibiwa kwamba Zanzibar kwa sasa haiwezi kupewa uanachama wa shirikisho hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa haina mamlaka ya kujiwakilisha yenyewe katika masuala ya michezo kimataifa, na hivyo iendelee kubebwa na mbeleko ya Tanzania kupitia Shirikisho la Soka (TFF).
Aidha, baada ya kupokea barua hiyo, uongozi wa ZFA kupitia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake Mzee Zam Ali, uliiandikia Wizara husika kuiarifu juu ya uamuzi huo wa FIFA, na baadae Waziri wa wizara hiyo
kuliambia Baraza la Wawakilishi kwenye kikao cha bajeti kilichopita kwamba ombi la Zanzibar limekataliwa.
Alipopigiwa simu Waziri Abdillahi Jihad Hassan ili atoe ufafanuzi endapo kuna majibu mapya kutoka FIFA yanayoipinga barua ya awali, simu yake haikuweza kupatikana kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment