Na Mwajuma Juma
TIMU ya soka ya New Boko, imeendelea kutoa takrima katika ligi daraja la pili taifa Unguja, baada ya juzi kusalimu amri mbele ya Super Stars kwa kuchapwa mabao 3-1.
Katika pambano hilo lililochezwa uwanja wa Polisi Ziwani, timu zote zilionesha ushindani mkali, lakini New Boko wakashindwa kudhihirisha ufundi wa katika kuzifumania nyavu.
Super Stars iliweza kujipatia mabao yake kupitia kwa wachezaji Said Mohammed aliyezichana nyavu mara mbili, dakika ya 39 na 61, huku Jabir Juma akimaliza hesabu ya mavuno kwa siku hiyo, mnamo dakika ya 42.
Bao la kufutia machozi kwa vijana wa Mwembenjugu, New Boko, lilifungwa na Salum Masoud dakika mbili kabla mchezo huo kufikia tamati.
Matokeo mengine ya ligi hiyo, Urafiki ikaifunga Shangani bao 1-0 katika uwanja wa Maungani, ambapo katika dimba la shimoni Mao Dzedong, wakati wa saa 8:00 mchana, Jumbi ikaifunga Mwakaje magoli 2-1.
Mchezo wa saa 10:00 uwanjani hapo, New Stars ikaramba mchanga kwa kupigwa mweleka wa mabao 2-1 na majirani zao wa karibu timu ya Coast Stars.
Aidha, watoto wa African Boys, wakaepuka upepo wa tufani kwa kuibugiza Kimbunga mabao 4-3, katika mchezo uliokuwa wa vuta nikuvute kwenye uwanja wa Fuoni.
No comments:
Post a Comment