Habari za Punde

WAHISANI WAOMBWA KUSAIDIA 'SOBER HOUSES'

Na Ramadhan Himid

WAHISANI wameombwa kutoa msaada wa hali na mali kwa vijana walioamua kuacha utumiaji wa dawa za kulevya ‘Tawabin Sober house” iliyoko eneo la Uzi Mjini Unguja ili kuwanusuru vijana dhidi ya athari za dawa za kulevya.

Mwenyekiti wa ‘Tawabin Sober house’, Ustadh Khatib Haji Seti alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Kamishna wa Polisi Zanzibar uliotembelea kuona mafanikio yaliyopatikana kwa vijana walioacha utumiaji wa dawa za kulevya.


Ustadh Khatib alisema kwamba katika Soba yao wamekuwa wakiwapa masomo mbali mbali wale walioamua kuacha utumiaji wa dawa za kulevya yakiwemo ya kimwili, kiakili na kiroho yakiwemo masomo ya Dini ya Kiislamu ili vijana hao warejee katika njia sahihi ya kuacha maovu na kumtumikia Mungu wao.

Alisema yeye mwenyewe binafsi kama mwanzilishi wa soba hiyo amekuwa akijitolea kuwasaidia vijana hao ambao kwa hiari yao wameamua kuachana na utumiaji wa dawa za kulevya lakini hali ya kiuchumi imekuwa ngumu na hivyo kuwaomba wahisani na wapenda maendeleo kutoa msaada wa hali na mali.

“Kubwa zaidi tunawaomba wahisani kutusaidia misaada mbali mbali , hasa ikizingatiwa kuwa soba yetu hii inatoa mafunzo kadhaa ikiwemo Dini ya Kiislamu ili kuwajenga vijana hao katika maadili mema na kuepukana na maovu ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya..’’, alisema Ustadh Khatib.

Akitoa nasaha zake kwa niaba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii, Mrakibu wa Polisi Ramadhan Khamis Salmin aliwaambia wana soba hao kwamba dawa za kulevya yanapoteza nguvu kazi ya taifa na hivyo kuwaomba wale wote waliojitolea kuacha dawa za kulevya waendelee na msimamo huo huo.

Alisema utumiaji wa hizo huchangia kuongezeka kwa makosa mbali mbali ya uhalifu nchini na hivyo kurejesha nyuma jitihada za Serikali katika kujiletea maendeleo.

Naye ofisa kutoka Kitengo cha Dawa zya Kulevya, Stesheni Sajenti Hamdani alisema serikali imeanzisha Sheria Na. 9 ya mwaka 2009 ya Madawa ya kulevya ili kupunguza vijana kutumia dawa hizo na sio kwa lengo la kuwafikisha jela kama wengi wao wanavyodhania.

Nao vijana waliopo katika soba hiyo wameliomba Jeshi la Polisi lifanye kazi zake kwa kuwashirikisha katika utendaji wa kazi zao kwani wao ndio wanaowafahamu wafanya biashara wa biashara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.