Habari za Punde

BALOZI WA TANZANIA NCHINI OMAN AMTEMBELEA MAALIM SEIF KUMUAGA


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na balozi mpya wa Tanzania nchini Oman Balozi Ali Ahmed Saleh huko nyumbani kwake Maisara Mjini Zanzibar. (Picha, Salmin Said-OMKR).

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali inakusudia kuyaendeleza maeneo huru ya kuchumi yaliyoko Fumba na Micheweni kwa kuyajengea mazingira bora ya uwekezaji.

Amesema katika kufikia hatua hiyo serikali inatafuta wafadhili wanakaoweza kuimarisha miundombinu ya kiuchumi katika maeneo hayo ili yaweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


Maalim Seif ameeleza hayo huko nyumbani kwake Maisara mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na balozi mpya wa Tanzania nchini Oman balozi Ali Ahmed Saleh aliyefika kwa ajili ya kumuaga kabla ya kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi nchini Oman.

Amesema iwapo maeneo hayo yataimarika kwa kuwekewa miundombinu inayostahiki ikiwemo barabara, umeme na maji safi na salama, yataweza kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi ambazo zisaidia kunyanyua pato la wananchi na taifa kwa jumla.

Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea haja kwa mamlaka ya kukuza vitega uchumi Zanzibar ZIPA kujipanga vizuri na kufanya kazi ya kuwavutia wawekezaji kulingana na mahitaji yaliyopo.

Wamesema katika kukuza diplomasia ya kiuchumi, ni vyema wawekezaji kujengewa mazingira mazuri yatakayoweza kuwashawishi, ikiwa ni pamoja na kurahisisha mawasiliano na kuwaondolea vikwazo vinavyoweza kurudisha nyuma mipango yao ya uwekezaji.

Pia viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuwepo mawasiliano na mashirikiano ya karibu baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje, ili kuwawezesha mabalozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

“ Ni kweli mabalozi wengi wanalalamika kuhusu jambo hili kuwa maombi mengi ya kibalozi wanayoyatuma serikalini huchumukua muda mrefu kujibiwa, jambo ambalo linazorotesha utendaji wao”, alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa atashauriana na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohd Shein ili nae ashauriane na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa lengo la kurekebisha kasoro hizo.

Kwa upande wake balozi Ali Ahmed Saleh ameahidi kuongeza bidii katika utendaji wake ili kuhakikisha kuwa uhusiano baina ya Oman na Tanzania unakua hadi kufikia kiwango kinachostahiki.

Balozi Saleh ameishauri serikali kutunza na kuilinda historia ya nchi, ikizingatiwa kuwa historia ni utajiri mkubwa kwa nchi husika.

Kabla ya balozi Saleh kuteuliwa hivi karibuni kuwa balozi wa Tanzania nchini Oman, alikuwa ni balozi mdogo wa Tanzania nchini Qatar katika falme za kiarabu.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.