Habari za Punde

BALOZI WA TANZANIA OMAN AMTEMBELEA BALOZI SEIF KUMUAGA


BALOZI mpya wa Tanzania Nchini Oman Bwana Ali Ahmed Saleh akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo ofisini kwake vuga mjini Zanzibar.
Balozi Saleh alikwenda kuagana Na Balozi Seif baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.


Upo umuhimu wa kuwekwa mikakati ya kuwepo kwa Kamati ya pamoja kati ya Tanzania na Oman kwa lengo la kuimarisha Ushirikiano wa muda mrefu wa pande hizo mbili.

Balozi wa Tanzania Nchini Oman Bw. Ali Ahmed Saleh ameeleza hayo alipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga kumuaga baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Oman hivi karibuni.


Balozi Ali Ahmed Saleh alisema hatua hiyo itasaidia kuunganisha vizuri Sekta zote katika mawasiliano ya pamoja ya ushirikiano baina ya sehemu mbili hizo.

Alifahamisha kwamba uteuzi wake umekuwa changamoto inayomkabili kutokana na Historia nzuri na rafiki kati ya Tanzania na Oman.

“ Kuna haja ya kuchukuliwa hatua zaidi ili daraja la uhusiano likasogezwa katika kiwango kikubwa zaidi ”. Alisisitiza Balozi Saleh.

Akizungumzia suala la Uwekezaji Balozi Saleh ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Kwa hatua yake ya kuendeleza Sekta ya Uwekezaji Vitega Uchumi Nchini.

Alisema ukosefu wa majibu ukiambatana na uchelewaji wa mikataba kwa baadhi ya wawekezaji unaelekea kuondoka kutokana na masuala hayo kupewa nafasi zaidi.

“ Inapendeza kuona masuala ya uwekezaji yamepewa nafasi zaidi katika kunyanyua uchumi wa Taifa ”. Alielezea faraja yake Balozi saleh.

Ameitaka Taasisi inayosimamia masuala ya uwekezaji Vitega Uchumi Hapa Zanzibar { zipa} kuwa wazi na makini katika uwajibikaji ili kuondoa mparaganyiko wa mapokezi ya Wawekezaji wanaopendelea kutaka kuwekeza Vitega Uchumi hapa Nchini.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amempongeza Balozi Ali Ahmed Saleh kwa kuteuliwa kwake kuwa Balozi wa Tanzania Nchini Oman.

Alisema na kuamini kwamba uteuzi huo utaleta faraja kwa Zanzibar kufaidika vyema na uhusiano wa Kihistoria uliopo kati yake na Oman kutokana na baadhi ya watu wake kuchanganya Damu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimuomba Balozi Saleh kuitangaza Nchini Oman Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo ya Zanzibar kwa lengo la kupata msukumo zaidi wa Maendeleo.


Othman Kahmis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/1/2012.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.