Habari za Punde

MASLAHI YA ZANZIBAR AFRIKA MASHARIKI YALINDWE : DK MWINYIHAJI

Na Rajab Mkasaba

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame amewataka Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Zanzibar kuhakikisha wanayalinda maslahi ya Zanzibar ndani ya Jumuiya hiyo.

Dk. Makame alieleza hayo ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Zanzibar ambapo mazungumzo hayo pia, yaliuhusisha uongozi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje.


Alisema kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kuendelea kutambulika pamoja na kuijua nafasi yake ndani ya jumuiya hiyo.

Alieleza kuwa Zanzibar ina mengi yanayopaswa kujulikana ikiwa ni pamoja na yanayotokea na yanayoendelea katika Jumuiya hiyo ambayo Zanzibar inapaswa kuyaelewa na kuyafanyia kazi.

Dk. Makame alieleza kuwa anafarajika kuona Wabunge wa Jumuiya hiyo kutoka Zanzibar wanafanya kazi kwa mashirikiano mazuri na wenzao kutoka nchi husika katika msimamo mmoja wa kuziletea maendeleo nchi
zao.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema kutokana na kutetea maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna haja kwa Jumuiya hiyo kufanya kazi katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ni
Zanzibar na Tanzania Bara ili mikakati na mipango ya maendeleo iweze kwenda sawia.

Waziri huyo alibainisha kuwa pamoja na Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana pamoja katika shughuli mbali mbali za kikazi. ‘Jisikieni mko nyumbani na karibuni sana wakati wowote mnakaribishwa hii pia, ni ofisi yenu karibuni sana”,alisema Dk. Makame.

Nao Wabunge hao akiwemo Dk. Said Gharib Bilal na Septuu Mohammed, walimueleza Waziri Makame kuwa Jumuiya hiyo imekuwa ikifanya kazi zake kwa mashirikiano ya pamoja kupitia wajumbe wake kutoka nchi zote tano wanachama.

Walieleza kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha nchi zote wanachama zinashirikiana katika kuimarisha na kuendeleza mikakati ya maendeleo ya kichumi, kijamii na kisiasa.

Walisema Zanzibar ina mengi ya mbali ya shughuli na mipango iliyowekwa na jumuiya hiyo pia, ipo haja kwa wananchi kupewa elimu ya kutosha juu ya Jumuiya hiyo na shughuli zake kwa Wajumbe wake.

Walieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kuifahamu Jumuiya hiyo, mipango yake, mikakati pamoja na uwajibikaji wa Wabunge hao katika uwakilishi wao kwenye Jumuiya hiyo.

Walieleza kuwa taratibu zimeshawekwa uliobaki ni utekelezaji kufuatia Azimio la Bujumbura juu ya Kiswahili cha Zanzibar kuwa ndio kiswahili sanifu na kuweza kutumika kitaifa na kimataifa.

Nao uongozi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje uliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa viongozi hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.