Habari za Punde

Wachezaji Wajibatiza Majina

Na Haji Nassor, Pemba

KUFUATIA kichapo cha magoli 4-3 mbele ya klabu ya Uwandani kwenye ligi daraja la pili taifa Pemba, timu ya Machomane imeilalamikia klabu hiyo kwa kuchezesha wachezaji mamluki.

Machomane (zamani Rungu) iliyowahi kucheza daraja la kwanza taifa, imetoa malalamiko yake hayo katika barua ya Novemba 24, 2011 iliyoituma kwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na kuwataja wanasoka wawili wa Uwandani kuwa walitumia majina bandia katika mchezo wao.


Barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wa Machomane FC Said Bakar, iliwataja wanandinga hao kuwa ni Omar Mnubi (kadi namba 4284), ambaye alidaiwa kuwa jina lake sahihi ni Zubeir Jaffar Juma.

Mwengine ni Salim Mkubwa mwenye kadi namba 4475, ambaye jina lake limeelezwa ndani ya barua hiyo kuwa ni Mustafa Jaffar Juma.

Aidha, barua hiyo imefahamisha kuwa, katika usajili wa mwaka 2010, wakati waliposajiliwa na klabu ya Small Yanga ya Vitongoji katika ligi daraja la pili Wilaya ya Chake Chake, wachezaji hao walitumia majina
yaliyotajwa na klabu hiyo kuwa ndiyo sahihi.

"Tumefuatilia kwa karibu na kubaini kuwa katika msimu uliopita, wachezaji hao walitumia majina ya Mustafa Jaffar Juma na Zubeir Jaffar Juma, lakini katika mchezo wetu wameorodheshwa kwa majina ya kufoji", ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Nakala ya barua hiyo, imetumwa pia kwa Katibu wa Kamati ya Rufaa Zanzibar, ZFA taifa Pemba pamoja na timu ya Uwandani F.C.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.