Habari za Punde

Simba Kufa Kupona leo

Na Mwandishi wetu

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa, timu ya Simba inashuka katika uwanja wa Taifa leo kuwakabili wageni wao timu ya Al Ahly Shandy kutoka Sudan katika mchezo wa kwanza wa 16 bora wa Kombe la Shirikisho.

Pambano hilo la leo ni muhimu kwa Simba, ambao wanatafuta nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Swaziland kuchezesha mechi hiyo.

Waamuzi hao wa mechi hiyo namba 71 ni Nhleko Simanga Pritchard atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake ni Mbingo Petros Mzikayifani na Sibandze Thulani.

Mwamuzi wa mezani atakuwa Fakudze Mbongiseni Elliot huku Kayijuga Gaspard wa Rwanda atakuwa Kamishna wa mechi hiyo.

Simba itahitaji kushinda mchezo huo ili ijiweke katika mazingira mazuri kabla ya pambano la marejeano litakalochezwa Mei 6 mjini Khartoum.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa shilingi, 5,000, 10,000, 15,000, 20,000 na 30,000, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Federick Sumaye.

Tayari uongozi wa Simba umewaomba mashabiki wote hasa wa mahasimu wao Yanga,kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti katika pambano hilo.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu amesema timu yake inahitaji sapoti ya Watanzania wote bila kujali tafauti zao za klabu hasa kwa kuwa wanaiwakilisha Tanzania.

“Kwa hatua tuliyofikia ni dhahiri nguvu za mashabiki zinahitajika ili kuwapa moyo wa ujasiri wachezaji,” alisema.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.