Tushirikiane utalii ulete manufaa kwa wote.
Awataka viongozi wa dini kusimamia mila, desturi.
Asema kasoro zinazoathiri zirekebishwe.
Na Salum Vuai, MAELEZO
Awataka viongozi wa dini kusimamia mila, desturi.
Asema kasoro zinazoathiri zirekebishwe.
Na Salum Vuai, MAELEZO
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema hakuna dini inayopinga biashara ya utalii, lakini ni muhimu maadili na tamaduni za nchi husika zilindwe na kupewa heshima yake.
Dk. Shein alitoa kauli hiyo jana alipofungua warsha ya siku moja iliyohusu dhana ya utalii kwa wote iliyofanyika katika ukumbi wa Salama hoteli ya Bwawani ikiwahusisha viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.
Alifahamisha kuwa dini ya Kiislamu, Kikristo na nyengine zilizopo Zanzibar, zinahimiza kufanya takrima kwa wageni, ambao kuja kwao nchini kunasaidia kuimarisha uchumi.
Hata hivyo, alishauri dhana za baadhi ya watu kuuona utalii kama tatizo, chanzo cha maovu, maasi na kuchangia katika kuvunja maadili na kuharibu tamaduni, zichunguzwe, akieleza matumaini yake kuwa warsha hiyo itatoa maoni na kupendekeza njia bora za kuufanya utalii wa Zanzibar uendane na maadili kwa manufaa ya watu wote.
Alisisitiza kuwa, lengo la serikali la kuleta utalii kwa wote, halikujikita katika kuzingatia manufaa peke yake, bali pia linazingatia jinsi wananchi na viongozi wote wanavyoweza kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya kuufanya utalii uwe na tija kwa jamii yote, na kuziondoa kasoro na madhara yanayosababishwa na jitihada zao za kuikuza sekta hiyo.
Hivyo, alieleza kuwa, viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi juu ya njia bora za kuwakaribisha wageni huku wakilinda dini, desturi na mila zao.
"Matumaini yangu kuwa, warsha hii itatoa miongozo bora itakayochangia katika jitihada za serikali za kukuza sekta hii bila ya kuharibu sifa njema tulizonazo za maadili mema ya wananchi wa visiwa hivi", alifafanua.
Akitoa ufafanuzi juu ya dhana ya utalii kwa wote, Dk. Shein alisema ni azma ya serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote wataendelea kufaidika na sekta hiyo, pamoja na kuzifanya sekta zote ziweze kushiriki na kutoa mchango wa moja kwa moja katika kuiendeleza sekta ya utalii.
Alifahamisha kuwa, hatua ya serikali kutafuta vyanzo vyengine vya kusaidia kuinua uchumi wake ikiwemo utalii, iliyotokana na msukosuko uliotokea baada ya kuangika kwa bei ya zao karafuu mnamo miaka ya 1970 na 1980.
Alisema kabla ya hapo, Zanzibar ilikuwa ikipokea kati ya watalii 25,000 na 40,000 kwa mwaka, na kufikia mwishoni mwa mwaka 2011, ilikisiwa kuwa watalii 175,000 waliingia nchini humu.
Aidha alieleza umuhimu wa kuyatumia kikamilifu majengo ya historia katika kuwavutia watalii wanaotaka kufahamu historia halisi ya Zanzibar, akitoa mfano wa nchi za Vatican, Uturuki, Italia, Hispania, Ufaransa na nyengine za Mashariki ya mbali, namna zinavyonufaika kutokana na kuviuza vivutio kama hivyo kwa watalii wanaozitembelea nchi hizo.
Alitaka majengo ya kale ya kidini kama vile msikiti wa Kizimkazi na kanisa la Anglikana Mkunazini, yatunzwe na kuendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kitalii na kuiingizia nchi pato la fedha za kigeni.
Alifahamisha, historia inaonesha kuwa, maendeleo ya Zanzibar na watu wake, yamefungamana na ufikaji wa wageni kutoka sehemu kadhaa za dunia waliofika kama watembezi na baadae kuanzisha makaazi ya kudumu.
Hali hiyo, alisema ndiyo msingi wa Zanzibar ya leo yenye utamaduni na desturi za pekee duniani, ambayo huonekana na kuthibitika popote pale.
"Tafiti mbalimbali za Kiakilojia (archaeology), zimethibitisha kufika kwa wageni Zanzibar katika karne nyingi zilizopita. Mwanahistoria wa Kiislamu katika karne ya 13 aliyeitwa Yakuut Al Hamawy ameandika kuwa Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha wasafiri na wageni hata kabla kuzaliwa Nabii Issa", alieleza Dk. Shein.
Aidha alisema vitabu mbalimbali vya kihistoria vimeandika juu ya kufika kwa wageni mbalimbali kutoka Bara la Ulaya wakiwemo ikina Captain James Lancaster waliofika Zanzibar mwaka 1592 kwa meli iliyoitwa 'Edward Bonaventure'.
Hata hivyo, aliwataka washiriki wa warsha hiyo na wananchi kwa jumla, kufahamu kuwa utalii ambao unategemewa sana kwa kukuza uchumi wa Zanzibar, hutegemea pia kuwepo kwa amani na utulivu pamoja na wenyeji wake kuheshimu na kukaribisha wageni.
Kuwepo kwa utulivu, alisema kunachangia kustawi kwa maisha ya wananchi, na kuelezea haja ya kuendelea kukumbushana juu ya umuhimu wake.
Mapema, akimkaribisha Rais Shein, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, alisema dhana ya utalii kwa wote, ina nafasi kubwa ya kuleta tija katika uchumi wa Zanzibar.
Aliwahimiza viongozi wa dini kuwashajiisha wafuasi wao na wananchi wa jumla kuiunga mkono, lakini pia kuhakikisha hawasahau mila na tamaduni zao ambazo zina sehemu kubwa katika kuwavutia watalii kuja nchini.
No comments:
Post a Comment