Na Salum Vuai, Maelezo
WACHEZAJI wawili waandamizi wa mchezo wa karate Zanzíbar, wameondoka jana kwenda nchini China kujifunza mbinu mpya ya ‘Chinese Shaolin Martial Art’.
Wanakarate hao waliosafiri kwa ndege ya Shirika la Ethiopian Airline, ni Khamis Abeid Khamis (kutoka staili ya Shotokan) pamoja na Salum Ali Saleh anayetokea katika staili ya Gujuru.
Akizungumza na gazeti hili, kabla ya kuondoka kwa wanamichezo hao, Mwenyekiti wa Chama cha Karate Zanzíbar Nassor Haji Nassor, alisema mafunzo hayo yatakayochukua miezi sita, yanafadhiliwa na Jamhuri ya Watu wa China katika ushirikano wake wa kimichezo na Zanzíbar.
Alieleza kuwa, mafunzo hayo ya Shaolin, yatakisaidia chama chake kuongeza staili ya tano ambayo itasajiliwa baada ya kurejea kwa wanamichezo hao, ambapo kwa sasa wanacheza karate kwa mitindo minne.
Alizitaja staili za sasa, kuwa ni Shaoring, Kombat, Gujuru na Shotokan.
Wakizungumza na Zanzíbar Leo kabla kupanda ndege, wapiganaji hao wa karate, waliahidi kuwa makini katika mafunzo hayo, ili waweze kujifunza vyema kwa manufaa yao na wanamichezo watakaokuja kuwafundisha watakaporejea nchini.
Naye Katibu wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzíbar (BTMZ) Hassan Khairallah Tawakal, aliishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa ushirikiano inaotoa kwa wanamichezo wa Zanzíbar, na kueleza matumaini yake kuwa itaendelea kutoa fursa zaidi kwa michezo mingine.
No comments:
Post a Comment