STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21.7.2012
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda amefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumpa mkono wa pole Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit hivi karibuni.
Spika Makinda ambaye alifuatana na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimueleza Dk. Shein kuwa wamefika Zanzibar kwa ajili ya kushiriki kutoa mkono wa pole ambapo tayari baadhi ya Wabunge walikwisha tangulia tokea majuzi.
Alisema kuwa viongozi wote hao wameguswa na tukio hilo na wanawapa pole wananchi wote wa Zanzibar kufuatia ajali hiyo na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa serikali zote mbili pamoja na wananchi wake.
Nae Dk. Shein alitoa shukurani kwa Spika huyo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ujumbe wake kwa niaba ya Wabunge wenzao na kueleza kuwa hatua hiyo inatia moyo sana.
Dk. Shein aliueleza ujumbe huo jinsi tukio hilo lilivyotokea sanjari na juhudi za Serikali zote mbili kupitia vyombo yake yva ulinzi na usalama pamoja na wananchi walivyoshiriki katika uokozi.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani wa vikosi vyote vya Serikali zote mbili pamoja na wananchi wakiwemo wamiliki wa vyombo vya baharini kwa kushiriki kikamilifu katika suala zima la uokozi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa hadi jana wameokolewa watu 145 ikiwa ni pamoja na kuopolewa maiti 68 hadi jana na kueleza kuwa miongoni mwa waliookolewa ni watalii 14 ambapo mmoja alifariki dunia kutokana na ajali hiyo.
Kutokana na tukio hilo Dk. Shein alisema kuwa Serikali zote mbili zinaangalia namna bora zaidi ya kujiandaa na zoezi la uokozi katika ajali kama hizo ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo zaidi katika matukio kama hayo.
Aidha, alisema kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha kasoro zilizokuwepo zinapunguzwa ama kuondoshwa kabisa ikiwa ni pamoja na uwezo mdogo, uhaba wa vifaa sanjari na utaalamu katika suala zima la uokozi.
Dk. Shein alisema kuwa waokoaji wamefanya kazi kubwa sana na kueleza kuwa ujio wa viongozi hao zinatokana na jitihada walizonazo pamoja na mapenzi kwa pande mbili za Muungano.
Wakati huo huo, salamu za rambi rambi zimeendelea kutolewa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Stagit na kusababisha vifo pamoja na majeruhi kadhaa.
Miongoni mwa salamu hizo za rambi rambi ni kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo katika salamu hizo chama hicho kilieleza kuwa kimepokea kwa majonzi, huzuni, masikitiko makubwa taarifa ya kuzama kwa meli ya MV Stagit.
Nae Umoja wa nchi za Ulaya (EU), umetoa mkono wa pole kwa Dk. Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar na kueleza kuwa ina unga mkono zoezi la uokozi na kufuatia ajali hiyo pia, Ubalozi wa Vietnam uliopo Tanzania, Ubalozi Mdogo wa India, Misri nazo zimetoa mkono wa pole.
Pamoja na hayo, Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania Nchini Misri, Japan na India nao walieleza jinsi walivyoshtushwa na taarifa ya kuzama kwa meli ya MV Stagit na kutoa pole kwa wale wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo.
Nayo Bodi ya Wakurugenzi na Wanachama wa Jumuiya ya Makampuni yanayotembeza Watalii Zanzibar (ZATO) wametoa mkono wa pole na kueleza jinsi walivyopokea kwa mshtuko tukio hilo.
Salamu hizo zilieleza kuwa msiba huo ni wa watu wote na wanamuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira wananchi katika kipindi hiki cha msiba, pia salamu hizo zilimuomba MwenyeziMungu majeruhi wote wa ajali hiyo wapone haraka ili wapate kurudi katika shughuli zao za kila siku za ujenzi wa Taifa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment